Rais wa Tunisia aigiza Tume ya Uchaguzi iandae uchaguzi wa Bunge
Rais wa Tunisia, Kais Saied ameitaka Tume Huru ya Uchaguzi nchini humo (ISIE) ifanye maandalizi ya uchaguzi wa Bunge uliopangwa kufanyika Disemba 17 mwaka huu.
Katika mazungumzo na Farouk Bouasker, Naibu Rais wa tume hiyo, Rais Saeid amesema ni jambo la dharura kwa taasisi hiyo kulinda uhuru wake, na kuwa na msimamo wa wastani katika utendaji kazi wake.
Amesema uchaguzi huo una umuhimu mkubwa kwa utulivu na muskatabali wa kisiasa wa Tunisia, hivyo Tume Huru ya Uchaguzi nchini humo ina jukumu kubwa la kuhakikisha kuwa uchaguzi huo unafanyika kwa mafanikio.
Jumatano iliyopita, Rais wa Tunisia alitangaza kuvunja Bunge muda mfupi baada ya chombo hicho kupitisha sheria ya kufuta hatua za dharura zilizotangazwa na kiongozi huyo Julai 25 mwaka jana.
Wakati huo, Rais huyo wa Tunisia alichukua uamuzi wa ghafla na wa kushangaza wa kusitisha shughuli za Bunge na kuwafuta kazi Spika na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, na kisha akatwaa udhibiti wa masuala yote ya utendaji nchini humo.
Wapinzani wake wamezitaja hatua hizo na nyinginezo ambazo zimekuwa zikichukuliwa na kiongozi huyo tokea wakati huo kuwa ni mapinduzi dhidi ya Katiba na dhidi ya mapinduzi ya wananchi yaliyouondoa madarakani utawala wa dikteta wa zamani wa nchi hiyo, Zine El Abidine Ben Ali.