Jun 01, 2016 06:59 UTC
  • Maandamano ya wanaopigania kujitenga eneo la kusini mwa Nigeria

Polisi katika jimbo la Niger Delta kusini mwa Nigeria wameeleza wasiwasi wao kuhusu kuongezeka maandamano ya wanaopigania kujitenga eneo hilo.

Polisi katika jimbo la Niger Delta kusini mwa Nigeria wamesema wanatiwa wasiwasi na maandamano ya wanaotaka kujitenga katika eneo hilo. Katika siku za hivi karibuni, watu kadhaa waliuliwa kufuatia maandamano yaliyofanywa na Harakati kwa jina la " Harakati ya Kuasisi Serikali Inayojitawala ya Biafra" katika eneo la Biafra na baada ya kujiri mapigano makali kati ya waandamanaji na polisi.

Hivi sasa pia kuongezeka mashambulizi katika taasisi na visima vya mafuta katika eneo la Niger Delta ni jambo linalotia wasiwasi. Eneo la Biafra katika nusu ya pili ya muongo wa sitini lilishuhudia vita vya umwagaji damu vilivyodumu kwa miaka miwili na miezi minane na kusababisha vifo vya watu karibu milioni moja. Kanali Ojukwu alitangaza kujipatia uhuru eneo la Biafra kwa kuungwa mkono na utawala wa Israel na Ufaransa.

Kugunduliwa mafuta huko Biafra na kuwepo harakati za baadhi ya makampuni ya kimataifa na serikali za nchi hizo kuyaunga mkono mashirika hayo ya uchimbaji mafuta, ilikuwa moja ya sababu kuu za kutokea vita katika eneo hilo. Uongozi wa Kanali Ojokwu ulidumu kuanzia tarehe 31 mwezi Mei mwaka 1967 hadi Januari mwaka 1970.

Ojukwu alikuwa akipata misaada kutoka nchi za Kikristo za Ulaya na Marekani, licha ya utawala wake kutambuliwa rasmi na nchi tano pekee wanachama wa Umoja wa Mataifa. Viongozi wa wakati huo wa Nigeria walituma jeshi na kulizingira kiuchumi eneo hilo na kumuangusha Kanali Ojukwu ambaye baadaye aliikimbia nchi.

Hata hivyo inaonekana kuwa licha ya kupita miaka mingi, matakwa ya raia wanaopigania kujitenga eneo hilo bado hayajazimika na bado kuna migawanyiko kati ya wananchi.

Mbali na kujiri machafuko hivi karibuni huko Biafra, harakati za waasi wa Harakati ya Ukombozi ya eneo la Niger Delta pia zimekuwa zikichagiza. Kuongezeka ghasia hizo, kumepelekea kunyooshewa kidole cha lawama Rais Muhamadu Buhari wa Nigeria. Baadhi ya pande zinapinga kuwa, kubadilika siasa za serikali tangu kuingia madarakani Rais Buhari hakuna uhusiano wowote na kuanza tena mizozo na machafuko.

Rais wa sasa wa Nigeria ameagiza kusakwa wahalifu baada ya kufuta makubaliano ya huko nyuma kati ya serikali na waasi wa Harakati ya Ukombozi ya Niger Delta. Hatua hiyo ya hivi karibuni imewapelekea waasi hao kutafuta vyanzo vipya vya kujipatia fedha. Hali ya mgogoro imepamba moto katika eneo tajiri kwa mafuta la kusini mwa Nigeria huku viongozi wa nchi hiyo wakikabiliwa na changamoto za kiuchumi zinazotokana na kupungua mapato ya mafuta, mashambulizi ya waasi wa kundi la Boko Haram katika maeneo ya kaskazini mwa nchi, kuwepo biashara ya mihadarati, mashambulizi ya maharamia katika Ghuba ya Guinea, mapigano na mizozo ya kidini katika jimbo la Bono linalopatika katika Ukanda wa Kati wa wa Nigeria na vile vile uingiliaji wa kigeni. Tunachopasa kushuhudia hivi sasa ni je Buhari atafanikiwa kuyapatia ufumbuzi matatizo ya Nigeria kwa kutumia nguvu ya jeshi na kupuuza chanzo cha matatizo hayo yote yanayorudisha nyuma maendeleo, kusababisha umaskini na ubaguzi nchini humo?

Tags