Algeria na Ufaransa zakubaliana kuanzisha ushirikiano mpya
Aug 28, 2022 02:36 UTC
Algeria na Ufaransa zimesaini tamko la pamoja la "ushirikiano mpya" mwishoni mwa ziara ya siku tatu ya Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa nchini Algeria.
Hati ya tamko hilo la pamoja ilitiwa saini na Rais wa Algeria Abdelmadjid Tebboune na Macron hapo jana wakati wa hafla iliyofanyika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Algiers.
Katika hafla hiyo, Tebboune alisema, ziara ya Rais wa Ufaransa nchini Algeria ilikuwa "bora, muhimu na yenye manufaa kwa mahusiano baina ya nchi hizo mbili."
Katika ziara ya rais Macron nchini Algeria, Paris na Algiers zimetia saini mikataba mitano ya ushirikiano katika masuala ya dawa, utafiti wa kisayansi, michezo na nyanja nyinginezo, sambamba na makubaliano yaliyofikiwa na serikali hizo mbili ya kuanzisha "ushirikiano wa kudumu" katika elimu ya juu na utafiti wa kisayansi.
Nchi hizo mbili zimekubaliana pia kuunda tume ya pamoja ya wanahistoria ili kutatua "kadhia ya kumbukumbu," inayohusiana na kipindi cha miaka 132 ya utawala wa kikoloni wa Ufaransa nchini Algeria kabla ya nchi hiyo kupata ushindi mwaka 1962 na kuwa taifa huru baada ya vita vya ukombozi vilivyochukua muda wa miaka minane.
Ziara ya rais wa Ufaransa nchini Algeria ilikuwa imelenga kupunguza mvutano uliokuwepo katika uhusiano wa pande mbili na kuimarisha ushirikiano baada ya nchi hizo mbili kumaliza mpasuko wa kidiplomasia mwezi Desemba mwaka jana uliokuwa umedumu kwa muda wa mwezi mmoja..../
Tags