Safari ya Waziri Mkuu wa Ufaransa nchini Algeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i89156-safari_ya_waziri_mkuu_wa_ufaransa_nchini_algeria
Jumapili ya juzi tarehe 9 Oktoba, Waziri Mkuu wa Ufaransa aliwasili katika mji mkuu wa Algeria Algiers akiuongoza ujumbe wa ngazi za juu wa nchi yake kwa ajili ya safari rasmi ya siku tatu katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 11, 2022 07:46 UTC
  • Safari ya Waziri Mkuu wa Ufaransa nchini Algeria

Jumapili ya juzi tarehe 9 Oktoba, Waziri Mkuu wa Ufaransa aliwasili katika mji mkuu wa Algeria Algiers akiuongoza ujumbe wa ngazi za juu wa nchi yake kwa ajili ya safari rasmi ya siku tatu katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Baada ya kuwasili mjini Algiers, Elisabeth Borne alilakiwa na mwenyeji wake Aimene Benabderrahmane, Waziri Mkuu wa Algeria. Safari ya Elisabeth Borne nchini Algeria ambayo inafanyika majuma kadhaa tuu baada ya safari ya Rais Emmanuel Macron inatathminiwa na weledi wa mambo kuwa, inalenga kujaribu kuboresha uhusiano uliodorora baina ya pande mbili hizo.

Safari hiyo inafanyika baada ya kuongezeka mvutano wa kisiasa kati ya nchi hizo kutokana na tafsiri na mitazamo tofauti kuhusu vita vya umwagaji damu vya kupigania uhuru wa Algeria. Mwishoni mwa mwaka jana, Algeria ilimwita nyumbani balozi wake kutoka Ufaransa kuhusiana na suala hilo hilo.

Mwezi Oktoba mwaka jana, Rais Emmanuel Macron aliushutumu "mfumo unaotawala wa kisiasa na kijeshi" wa Algeria kwa kutumia kumbukumbu za vita vya uhuru kuendeleza uhai wake na kuhalalisha uwepo wake. Macron pia alihoji kuwepo kwa "taifa la Algeria kabla ya ukoloni wa Ufaransa" na kusisitiza haja ya kushughulikia suala hilo ili kuleta "maelewano kati ya wananchi".

Elisabeth Borne, Waziri Mkuu wa Ufaransa (kushoto) akiwa na mwenyeji wake nchini Algeria

 

Hii ni katika ahali ambayo, kuna nyaraka nyingi za kihistoria zinazoonyesha kuwa, katika kipindi cha kuikoloni Algeria, Ufaransa ilifanya jinai kubwa dhidi ya Waalgeria huku ikipora rasilimali zao, pamoja na kufanya majaribio ya nyuklia katika ardhi ya nchi hiyo kwa madhara ya wakaazi wake. Kwa hivyo, viongozi wa Algeria mara kwa mara wamekuwa wakitaka nchi hiyo kuombwa msamaha rasmi na viongozi wa Paris. Lakini viongozi wa Ufaransa wamekuwa wakikwepa kuomba msamaha, hatua ambayo imeendelea kuzorotesha uhusiano wa pande mbili.

Pamoja na hayo katika miezi ya hivi karibuni na kufuatia kutokea mabadiliko ya kisiasa katika uga wa kimataifa, kuibuka vita vya Ukraine na kupungua usafirishaji wa gesi ya Russia kuelekea Ulaya, hivi sasa mataifa ya Ulaya yamo mbioni kufanya mazungumzo na mataifa mengine yanayosafirisha nishati nje ya nchi hususan barani Afrika. Katika uwanja huo, kuboreshwa uhusiano na kupanuliwa wigo wa biashara na Algeria ikiwa mshirika mkongwe wa kibiashara wa Ufaransa kwa mara nyingine tena ni jambo ambalo limewekwa katika ajenda ya viongozi wa Paris.

Ni kwa kuzingatia ukweli huo, ndio maana Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa alisema mwishoni mwa safari yake mwezi Agosti mwaka huu kwamba: Tuna uhakika juu ya kudhaminiwa Ufaransa nishati katika msimu huu wa baridi kali, na Algeria pia bila shaka itataka kuwa na vyanzo tofauti vya kujidhaminia mapato yanayotokana na uuzaji wa gesi katika nchi za Ulaya.

Algeria haizingatiwi tu kwa sababu ya kuwa na akiba ya kubwa ya mafuta na gesi, bali jambo jingine ni kutokana na nchi hiyo kuwa na mabomba ya gesi ambayo yanayounganisha nchi hiyo na Italia na Uhispania hasa katika kipindi hiki ambacho kuna uhaba mkubwa wa nishati barani Ulaya. Hali hiyo ya Algeria imezifanya nchi nyingine za Ulaya kuhaha huku na kule ili kuhakikisha kuwa zinaimarisha uhusiano na Algeria ili kuandaa mazingra ya kutiliana saini mikataba mbalimbali na nchi hiyo ambayo kijiografia ipo kaskazini mwa Afrika.

Marais wa Ufaransa na Algeria walipofanya mazungumzo mwezi Agosti mwaka huu (2022) mjini Algiers

 

Wajuzi wa mambo wanaamini kuwa, hata kama rasilimali ya gesi ya Algeria haiwezi kuziba kabisa pengo lililoachwa wazi na Russia, lakini bila shaka itakuwa na nafasi muhimu katika kukidhi mahitaji ya nishati ya Ulaya kadiri muda unavyosonga mbele.

Hata hivyo nafasi ya kijeshi na kiusalama ya Ufaransa barani Afrika, ni jambo jingine linalotiliwa maanani na viongozi wa Paris katika kukuza na kuimarisha uhusiano wa nchi yao na Algeria. Baada ya Ufaransa kuondoa wanajeshi wake katika baadhi ya mataifa ya Kiafrika kama Mali, na kushadidi mzozo kuhusu utendaji wa vikos hivyo, filahi Ufaransa kabla ya kitu kingine inafuatilia suala la kuweko kijeshi katika nchi kama Algeria.

Hilo linatokana na kuwa, stratejia mpya yoyote kuhusiana na usalama wa nchi ya Mali na eneo, inapaswa kufanyika kwa uratibu na Algeria. Hasa kwa kutilia maanani kuwa, hali ya usalama nchini Mali kama ilivyo kwa Libya ni jambo lenye umuhimu mkubwa kwa uthabiti wa Algeria. Fauka ya hayo, uwepo wa washindani kama Russia na China huko barani Afrika ni jambo jingine ambalo limewatia kiwewe viongozi wa Ufaransa.