Burkina Faso yasimamisha matangazo ya redio ya RFI ya Ufaransa
Serikali ya Burkina Faso imesimamisha nchini humo matangazo ya Redio ya Kifaransa ya RFI inayofadhiliwa na serikali ya Paris, kwa madai ya kutangaza habari za uwongo na upotoshaji.
Serikali ya kijeshi ya Burkina Faso inakituhumu chombo hicho cha habari cha Ufaransa kuwa kinaripoti habari za uwongo na kuyapa jukwaa na sauti magenge ya kigaidi.
Taarifa iliyotolewa jana Jumamosi na serikali ya Burkinabe imeeleza kuwa, RFI ilirusha hewani ujumbe wa kiongozi mmoja wa genge la kigaidi, ambapo alitishia usalama wa taifa la Burkina Faso.
Kinara wa genge la kigaidi la Jama’a Nusrat ul-Islam wa al-Muslimin (JNIM) lenye mfungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda alisikika akitoa vitisho dhidi ya raia wa Burkina Faso wanaojitolea kuunga mkono operesheni za serikali dhidi ya magenge ya kigaidi.
Machi mwaka huu pia, nchi nyingine ya Afrika Magharibi, Mali, ilichukua hatua ya kusitisha nchini humo matangazo ya Redio ya Kifaransa ya RFI na televisheni ya France 24 kwa tuhuma kuwa vyombo hivyo vya habari vinaripoti habari za uwongo na upotoshaji. Mashirika hayo ya Ufaransa yalidai kwamba jeshi la Mali limeua makumi ya raia.
Siku chache zilizopita, Baraza la Kijeshi la Mali lilipiga marufuku shughuli zote za mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo yanafadhiliwa kifedha na Ufaransa.
Uhusiano wa Mali na Ufaransa uliharibika tangu jeshi lilipoingia madarakani katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi mwaka 2020, na vile vile kufuatia matamshi ya kiadui na kichochezi ya Paris; huku hisia za chuki dhidi ya Ufaransa zikiongezeka katika eneo zima la Sahel.