Tahadhari kuhusu kujiimarisha Daesh huko Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i925-tahadhari_kuhusu_kujiimarisha_daesh_huko_libya
Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuhusu juhudi za kundi la kigaidi la Daesh za kuimarisha ushawishi wake huko Libya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 09, 2016 22:12 UTC
  • Mjumbe wa UN Libya na kamanda wa Jeshi wa nchi hiyo
    Mjumbe wa UN Libya na kamanda wa Jeshi wa nchi hiyo

Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuhusu juhudi za kundi la kigaidi la Daesh za kuimarisha ushawishi wake huko Libya.

Martin Kobler Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya amesema kuwa ipo hatari ya kuimarika ushawishi wa magaidi wa Daesh katika maeneo mengi ya Afrika na kundi hilo kujiunga na lile la Boko Haram huko Nigeria, Niger na Chad.

Kobler ametahadharisha kuhusu kuzidi kujiimarisha magaidi wa kundi la Daesh katika maeneo mengine ya Libya na kutaka kuundwa haraka iwezekanavyo serikali ya umoja wa kitaifa nchini humo.

Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya jana pia alisema kuwa wananchi wa Libya wanasubiri kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa ili kufanikishwa malengo yao. Martin Kobler ametahadharisha pia kuhusu kupuuzwa hali ya mambo ya Libya na kueleza kuwa raia wa nchi hiyo wanataraji kuwa serikali ya umoja wa kitaifa itaundwa kama ilivyopangwa huku wakiwa na matarajio makubwa kutoka kwa serikali hiyo. Wawakilishi wa bunge la Libya linalotambuliwa rasmi na jamii ya kimataifa lenye makao yake mashariki mwa nchi hiyo na bunge jingine lenye makao yake huko Tripoli katikati ya mwezi Disemba mwaka jana walisaini makubaliano nchini Morocco chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa kwa minajli ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa nchini humo. Serikali ya umoja wa kitaifa ya Libya inatazamiwa kuarifishwa bungeni wiki ijayo.