Baada ya kutimuliwa Ufaransa, magaidi 160 waangamizwa Burkina Faso
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i94292-baada_ya_kutimuliwa_ufaransa_magaidi_160_waangamizwa_burkina_faso
Magaidi wasipoungua 160 wameangamizwa katika operesheni ya jeshi la Burkina Faso katika eneo la Sahel, wakati huu ambapo mabaki ya askari vamizi wa Ufaransa wanaendelea kuondoka nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 21, 2023 04:01 UTC
  • Baada ya kutimuliwa Ufaransa, magaidi 160 waangamizwa Burkina Faso

Magaidi wasipoungua 160 wameangamizwa katika operesheni ya jeshi la Burkina Faso katika eneo la Sahel, wakati huu ambapo mabaki ya askari vamizi wa Ufaransa wanaendelea kuondoka nchini humo.

Taarifa ya jeshi hilo imeongeza kuwa, maiti zaidi ya 60 za wanamgambo waliotekeleza shambulizi la kushtukiza dhidi ya kambi za kijeshi baina ya maeneo ya Deou na Oursi katika mkoa wa Oudalan, zimepatikana katika eneo hilo. Hata hivyo duru nyingine za kijeshi zimesema idadi ya magaidi walioangamizwa kwenye operesheni hiyo ni 160.

Habari zaidi zinasema kuwa, kufikia jana Jumatatu, wanajeshi 51 wa Burkina Faso walikuwa wameangamizwa kwenye makabiliano hayo yaliyoanza tangu Ijumaa iliyopita.

Taarifa ya Idara ya Mawasiliano na Uhusiano Mwema ya Jeshi la Burkinabe imesema vikosi vya usalama vya nchi hiyo vimepata mafanikio makubwa katika operesheni zao ndani ya wiki chache zilizopita, ambapo mamia ya magaidi wameuawa.

Kuondoka mabaki ya askari vamizi wa Ufaransa nchini Burkina Faso

Haya yanajiri wakati huu ambapo wananchi wa Burkina Faso wanaendelea kufurahia na kumiminika mabarabarani kwa shangwe kufuatia taarifa ya kufikia tamati uwepo wa wanajeshi wa Ufaransa katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Mwezi wa Januari mwaka huu, Burkina Faso iliipa Ufaransa mwezi mmoja iwe imeondoa vikosi vyake wakati ikimaliza makubaliano ya kijeshi, yaliyoruhusu vikosi vya Ufaransa kupambana na waasi katika himaya yake, ikielezea kuwa nchi itajilinda yenyewe.

Maelfu ya watu wameuawa na wengine zaidi ya milioni mbili wamekimbia makazi yao tangu magaidi hao wakufurishaji waanze kuishambulia Burkina Faso kutokea nchi jirani ya Mali mnamo 2015.