Feb 25, 2023 02:43 UTC
  • Raia 12 wauawa katika shambulizi la wabeba silaha nchini Mali

Kwa akali raia 12 wameuawa katika shambulizi la watu waliojizatiti kwa silaha katikati ya Mali.

Hayo yameripotiwa na maafisa wawili wa serikali waliozungumza na shirika la habari la Reuters jana Ijumaa, na kusema kuwa shambulio hilo lilitokea Alkhamisi katika kijiji cha Bankass Circle, eneo la Mopti, katikati ya Mali.

Meya wa mji wa Bankass, Moulaye Guindo amesema watu waliokuwa na silaha walivamia kijiji hicho na kuanza kuwafyatulia risasi ovyo wanakijiji na kuwaua.

Kwa mujibu wa meya huyo, maiti 19 zimepatikana kufikia sasa, huku shughuli ya kusaka miili zaidi ikiendelea, kwani kuna baadhi ya wanakijiji walitorokea katika msitu wa karibu.

Naye meya wa mji wa Kani Bonzon ulioko jirani na eneo la tukio, Soumaila Guindo, amesema hospitali ya kijiji kilichoshambuliwa kimepokea maiti 12 kufikia sasa.

Askari wa Ufaransa waliotimuliwa Mali wakituhumiwa kuunga mkono magenge ya kigaidi

Amesema wavamizi hao mbali na kuua wanakijiji, lakini wamechoma moto pia nyumba zao na kusababisha uharibifu mkubwa. Mali imekumbwa na hujuma za makundi na magenge yenye silaha yenye mfungamano na al Qaida na Daesh tokea mwaka 2012.  

Jumanne iliyopita, askari wa kulinda amani watatu wa Umoja wa Mataifa waliuawa na wengine watano walijeruhiwa wakati msafara wao ulipogonga bomu la kutegwa barabarani (IED) katikati mwa Mali. Hayo yalisemwa na ujumbe wa Umoja wa Mataifa katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

 

Tags