Burkina Faso yavunja rasmi makubaliano ya kijeshi ya 1961 na Ufaransa
Burkina Faso imevunja rasmi makubaliano ya kijeshi iliyosaini na Ufaransa mwaka 1961, wiki chache baada ya kumtaka mkoloni wake huyo wa zamani kuondoa vikosi vyake na balozi wake nchini humo.
Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, serikali ya Ufaransa ilipokea rasmi jana Jumatano arifa ya kuvunjwa makubaliano hayo ya kijeshi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Burkina Faso.
Ufaransa imekuwa ikitumia makubaliano hayo ya msaada wa kiufundi wa kijeshi yaliyofikiwa baina pande mbili mnamo Aprili 24, mwaka 1961, kuhalalisha uwepo wake nchini Burkina Faso.
Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Februari, mabaki ya wanajeshi wa Ufaransa walianza kuondoka nchini Burkina Faso na kuhitimisha uwepo wao katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika uliodumu kwa miaka 10.
Uamuzi wa Burkina Faso wa kuwatimua wanajeshi wa Ufaransa ni ushahidi wa kuzidi kuzorota uhusiano kati ya Ufaransa na koloni lake hilo la zamani baada ya mapinduzi ya kijeshi ya mwezi Septemba 2022.
Wadadisi wa mambo wanaamini kuwa, uwepo wa jeshi la Ufaransa nchini Burkina Faso haujaimarisha usalama katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Aidha wananchi wa Burkina Faso wanaamini kwamba, ni wakoloni hao wa Ulaya ambao wanachochea machafuko, mapinduzi ya mfululizo ya kijeshi, vitendo vya kigaidi na ukosefu wa usalama nchini humo.