Burkina Faso yaifungia 'France 24' baada ya mahojiano na al-Qaeda
Serikali ya kijeshi ya Burkina Faso imesimamisha matangazo ya kanali ya televisheni ya Ufaransa ya France 24, baada ya chombo hicho kurusha hewani mahojiano kiliyoyafanya na kiongozi wa kundi la kigaidi la al-Qaeda tawi la Kaskazini mwa Afrika AQIM.
Jean-Emmanuel Ouedraogo, Waziri wa Mawasiliano wa Burkina Faso amesema katika taarifa kuwa, "France 24 si tu imegeuka na kuwa msemaji wa hawa magaidi, lakini mbaya zaidi, imekuwa uwanja wa kuhalalisha vitendo vya kigaidi na matamshi ya chuki."
Mapema mwezi huu, kanali ya televisheni ya Ufaransa ya France 24 ilipeperusha mahojiano iliyoyafanya na mtu anayejiita Amir wa al-Qaeda, Yazid Mubarak, ambaye anafahamika pia kama Abu Ubaydah Yusuf al-Anabi.
Stesheni hiyo ya Ufaransa tayari imefungiwa katika nchi za Mali na Algeria kwa ama kurusha hewani habari za urongo na upotoshaji, au kuwapa magaidi uwanja wa kujifaragua na kuhalalisha harakati zao.
Burkina Faso na mkoloni wake huyo wa zamani wa Ulaya zimekuwa zikivutana na kulumbana kwa miaka mingi sasa juu ya mambo mbali mbali.
Mapema mwezi huu, Burkina Faso ilivunja rasmi makubaliano ya kijeshi iliyosaini na Ufaransa mwaka 1961, wiki chache baada ya kumtaka mkoloni wake huyo wa zamani kuondoa vikosi vyake na balozi wake nchini humo.
Uhusiano kati ya Ufaransa na Burkina Faso umeharibika sana tangu yalipotokea mapinduzi ya kijeshi ya mwezi Septemba 2022 katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.