May 13, 2023 07:22 UTC
  • Makubaliano ya awali ya pande zinazozozana Sudan kwa ajili ya kusitisha mapigano

Hatimaye baada ya siku tatu za mazungumzo magumu ya kurudisha amani nchini Sudan, pande mbili zinazohasimiana zimetia saini taarifa na kukubaliana kuwa maslahi ya watu wa nchi hiyo yapewe kipaumbele. Pande hizo zimekubali kuchukua hatua zote za lazima ili kutowadhuru raia na kuwaruhusu waondoke kwenye maeneo yenye mapigano na yaliyozingirwa.

Kwa msingi huo, pande hizo zimeahidi kutoharibu mali ya umma na ya kibinafsi nchini Sudan na kusaidia wafanyikazi wa afya kutekeleza majukumu yao na pia kuwalinda raia. Vile vile jeshi la Sudan na kikosi cha radiamali ya haraka wamekubaliana kusimamisha mapigano kwa ajili ya kuruhusu shughuli za kibinadamu katika nchi hiyo na kujiepusha kutumia watoto katika vita.

Faisal bin Farhan, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, ambaye nchi yake imekuwa mpatanishi katika mazungumzo hayo amesema kwamba suala muhimu ni kushikamana wahusika na yale yaliyoafikiwa katika mazungumzo hayo.

Mapigano kati ya vikosi vya jeshi la Sudan chini ya uongozi wa Jenerali Abdul Fattah al-Barhan ambaye pia ni mkuu wa Baraza Tawala la Sudan na Mohammed Hamdan Deglu aliyepewa jina la utani la "Hamidti" kamanda wa Kikosi cha Radiamali ya Haraka huko Khartoum, mji mkuu wa Sudan, yameingia katika wiki ya nne. Hii ni katika hali ambayo mali nyingi za umma katika mji mkuu zimeharibiwa na raia wengi wamelazimika kusalia nyumbani au kukimbilia katika nchi jirani ili kulinda usalama wao.

Mapigano mjini Khartoum

Hata kama juhudi kubwa za upatanishi kutoka ndani na nje ya Sudan zilifanyika mwanzoni mwa mapigano ili kuyasimamisha, lakini juhudi hizo hazikufua dafu. Al-Barhan na Hamidti, ambao wanatuhumiana kuanzisha mapigano hayo, wanaamini kwamba wanaweza kushinda vita na hatimaye kuchukua madaraka ya nchi, kwa hivyo, hawakubali kusitisha mapigano moja kwa moja.

Umoja wa Mataifa sasa unakadiria kuwa watu milioni 5 nchini Sudan wanahitaji msaada wa dharura ambapo miundombinu ya afya na matibabu ya nchi hiyo imeporomoka.

Crystal Wells, Msemaji wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu, amesema hospitali nyingi za Sudan zimekuwa hazina umeme wala maji kwa siku nyingi mfululizo na sasa zinasubiri msaada wa dharura. Ameongeza kwamba hali ya lishe duni na uhaba wa chakula nchini Sudan ni mbaya sana.

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani pia limetangaza kuwa watu milioni 2.5 wanatarajiwa kukabiliwa na baa la njaa nchini Sudan katika siku za usoni kutokana na ghasia, jambo ambalo litaathiri pakubwa usalama wa chakula nchini na kuufanya kuwa katika kiwango cha chini kabisa.

Hali hiyo imewapelekea wahusika wakuu wa mzozo Sudan hatimaye kukubali kutia saini makubaliano hayo katika saa za mwisho za mazungumzo. Madhumuni ya makubaliano hayo ya muda ya kusitisha mapigano ni kuwezesha ufikishaji wa misaada ya dharura ya kibinadamu na kukubaliana juu ya ratiba ya mazungumzo ya usitishaji vita wa kudumu.

Dk. Mohammad Al-Salami, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema: Chaguo bora kwa pande zote mbili ni kukubali mazungumzo na kuyachukulia kuwa chombo cha kusimamisha mapigano ya sasa, ili kuyazuia kuongezeka, na hivyo kuondoa tishio la kugawanyika zaidi nchi hiyo.

Hali mbaya ya mgogoro wa Sudan na kuendelea vita sio tu ni hatari kubwa kwa nchi hiyo bali pia kwa nchi zingine za eneo hilo. Hivi sasa, wakimbizi wa Sudan wamekimbilia katika nchi jirani, na wengi wanasubiri kuanzishwa usitishaji vita na njia salama za kukimbia kutoka kwenye maeneo ya vita.

Abdullah Hamdok

Abdullah Hamdok, Waziri Mkuu wa zamani wa Sudan, pia amesema vita vinapasa kusimamishwa bila kuchelewa na kuandaliwa mazingira ya amani mara moja. Anasisitiza kuwa amani ndilo chaguo pekee kwa watu wa Sudan.

Hata kama hatua ya kwanza ya usitishaji vita nchini Sudan imekwishachukuliwa na wahusika wamekubali kuitekeleza, lakini kuheshimiwa na kutekelezwa kwake kivitendo ni suala jingine litakalothibitishwa au kukanushwa kadiri muda unavyopita. Wananchi wa Sudan wanatarajia kurejea amani katika nchi yao, hata kama hilo linaonekana kuwa jambo lililo mbali kufikiwa kwa sasa.

Tags