Wasudan wakasirishwa na kupewa Saudia ardhi ya nchi yao
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i9802-wasudan_wakasirishwa_na_kupewa_saudia_ardhi_ya_nchi_yao
Kitendo cha bunge la Sudan cha kupasisha makubaliano ya Khartoum na Riyadh ya kupewa Saudi Arabia haki ya kutumia hekari laki moja za ardhi ya kaskazini mwa Sudan, kimelalamikiwa vikali na wananchi wa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 23, 2016 11:23 UTC
  • Wasudan wakasirishwa na kupewa Saudia ardhi ya nchi yao

Kitendo cha bunge la Sudan cha kupasisha makubaliano ya Khartoum na Riyadh ya kupewa Saudi Arabia haki ya kutumia hekari laki moja za ardhi ya kaskazini mwa Sudan, kimelalamikiwa vikali na wananchi wa nchi hiyo.

Televisheni ya al Alam imeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, bunge la Sudan limepasisha makubaliano yaliyotiwa saini baina ya Khartoum na Riyadh, makubaliano ambayo yanaupa haki ukoo wa Aal Saud wa Saudi Arabia kutumia hekari laki moja zenye rutba za kaskazini mwa Sudan kwa muda wa miaka 99.

Hata hivyo baadhi ya wachambuzi wa mambo wamesema kuwa, makubaliano hayo ni katika kuvutia uwekezaji wa nchi za Kiarabu, lakini hatua ya bunge la nchi hiyo ya kupasisha makubaliano hayo imelalamikiwa vikali ndani ya Sudan.

Wapinzani wa hatua hiyo wanasema kuwa, makubaliano hayo yatawafanya wakimbizi wakazi wa maeneo ya kaskazini mwa Sudan ambao wanatumia kilimo kama njia yao kuu ya kupatia rizki.

Sudan ina karibu hekari milioni 20 zinazofaa kwa kilimo na hiyo ni sawa na asilimia 45 ya ardhi inayofaa kwa kilimo katika ulimwengu mzima wa Kiarabu.