Spoti, Agosti 18
Natumai u mzima msikilizaji mpenzi. Karibu tuangazie baadhi ya matukio muhimu ya spoti yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita katika pembe mbali mbali za dunia.
Mieleka; Iran yavuna medali lukuki
Iran imeibuka bingwa wa mashindano ya kimataifa ya mieleka aina ya Greco-Roman baada ya kushinda medali 3 za dhahabu, medali 1 ya fedha, na medali 4 za shaba. Mashindano hayo ya kimataifa ya mieleka ya Greco-Roman kwa jina la Kombe la Ljubomir Ivanovic Gedza yalifanyika Mladenovac, Serbia.

Katika mashindano hayo ya Kombe la Ljubomir Ivanovic Gedza, yaliyoshirikisha wanamieleka kutoka nchi zinazoongoza duniani, zikiwemo Serbia, Bulgaria, Hungary, Kyrgyzstan, Sweden, Romania, Kroatia na Belarus, raia wa Iran, Mohammad Pouya Asadi katika kitengo cha uzani wa kilo 55, Reza Gheitasi katika kilo 63 na Mohammad Hosse kg 80 walishinda medali za dhahabu . Wakati huo huo, Iman Mohammadi katika daraja la kilo 72 aliinyakulia Iran medali ya fedha, huku Amir Mehdi Saeedi Nava katika kilo 77, Alireza Mohammad Hosseini kilo 82, Yassin Yazdi kilo 87, na Ayoub Hosseinvand katika kilo 130 wakitwaa medali 4 za shaba.
Basketboli Asia: Iran mshindi wa 3
Iran iliizidi kete New Zealand na kupata ushindi wa vikapu 79-73 katika mchezo wa kusaka mshindi wa tatu wa Kombe la FIBA Asia 2025 Jumapili katika Uwanja wa Mfalme Abdullah Sports City, na kuibuka tena kwenye jukwaa baada ya kukosa 2022. Mshambulizi mkongwe Arsalan Kazemi alizoa pointi 16, ribaundi 15 na vikapu vitatu kwa mpigo, huku Mehdi Jafari aking'ara zaidi akiwa na pointi 22, asisti 5 na pointi tatu. Mlinzi Sina Vahedi aliongeza pointi 19, ribaundi 5 na asisti 4 huku Timu ya Melli ikimaliza na rekodi ya 5-1 sajnari na kutwaa medali ya shaba.

Kwa Iran, matokeo yaliashiria kurudi kwa fahari kwenye jukwaa la FIBA Asia Cup, na kuimarisha hadhi yao kati ya mamlaka ya kudumu ya kanda. Baada ya kuangukia kwa mabingwa watetezi Australia katika Nusu Fainali, Timu Melli ilijibu kwa ujasiri na kumaliza nafasi ya tatu kwa jumla. Kwa ushindi huu, Iran inaweza kuondoka Saudi Arabia ikiwa imeridhika na vifaa vya mkononi na hali ya juu iliyorejeshwa. Kwa kikosi cha Kocha Sotirios Alex Manolopoulos, kumaliza katika nafasi ya tatu kunatoa ukumbusho wa ukoo wao, na jukwaa la kujenga kwa ajili ya kizazi kipya.
Robo Fainali CHAN
Timu ya taifa ya soka ya Kenya 'Harambee Stars' siku ya Jumapili ilituama kileleni mwa Kundi A katika kindumbwendubwe cha Kombe la Afrika kwa wachezaji wanaoshiriki Ligi za Nyumbani (CHAN 2024) baada ya kuitandika Zambia bao 1 la uchungu bila jibu katika Uwanja wa Kasarani jijini Nairobi. Mshambuliaji Ryan Ogam alifunga bao hilo dakika ya 75 na kuwaamisha mashabiki 27,000 ambao walikuwa Kasarani akiwemo Rais William Ruto na Kinara wa ODM Raila Odinga. Kiungo Boniface Muchiri alikuwa amepokea pasi kutoka kulia, akaenda na mpira hadi katikati mwa uwanja na kummegea pasi Ogam ambaye hakuwa ameandamwa na mchezaji yoyote. Sajili huyo mpya wa Gor Mahia aliudhibiti mpira na kuachilia fataki ambayo ilimlemea kipa wa Zambia kunyaka na kuamsha umati ambao ulikuwa unashangilia vijana wa nyumbani.

Ushindi huo ulihakikisha Kenya inamaliza juu ya Kundi A kwa alama 10, na sasa itacheza robo fainali dhidi ya Madagascar Ijumaa hii hapa nchini. Morocco ilimaliza nambari mbili katika kundi hilo baada ya kuitandika Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DR Congo) 4-1 katika mechi nyingine ugani Nyayo. Kenya ingecheza dhidi ya Tanzania iwapo haingeshinda mechi hiyo kwa kuwa wangemaliza nambari mbili kundi lao. Angola walibanduliwa wakiwa na alama nne huku Zambia ikiwa haina alama zozote baada ya kupoteza mechi zake kundi A. Morocco sasa itacheza dhidi ya Tanzania ugenini kwenye mechi nyingine ya robo fainali baada ya kumaliza nambari mbili. Ushindi huo pia umenufaisha wanasoka wa Harambee Stars kifedha kwa kuwa watapokea Sh2.5 milioni kwa kila mchezaji jinsi walivyoahidiwa na Rais William Ruto.
Siku ya Jumamosi, timu ya Taifa ya soka ya Tanzania ‘Taifa Stars’, ilimaliza mechi zake za makundi fainali za CHAN 2024 kwa kutoka 0-0 na Jamhuri ya Afrika ya Kati mchezo uliopigwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam. Kutokana na matokeo hayo Taifa Stars imemaliza Kundi B ikiongoza kwa pointi 10 sawa na Kenya katika kundi lake A, baada ya kushinda michezo mitatu ya mwanzo. Wachezaji, wasimamizi na mashabiki wa Taifa Stars wameridhishwa na mwenendo mzima wa vijana wa nyumbani. Kiungo wa Tanzania, Feisal Salum 'Fei Toto' anaeleza kilichowamnyima bao kwenye mechi hiyo.

Madagascar imeshika nafasi ya pili ikiungana na Stars kucheza robo fainali baada ya kuifunga Burkina Faso mabao 2-1, hivyo kufikisha pointi 7 sawa na Mauritania isipokuwa Madagascar ina uwiano mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Wakati huo huo, Bodi ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) imeipiga Kenya faini ya dola 50,000 za Marekani kutokana na makosa ya kiusalama yaliyojitokeza katika mchezo dhidi ya Morocco uliofanyika kwenye Uwanja wa Moi, Kasarani. CAF imeonya kuwa iwapo kasoro hizo zitaendelea, mechi zijazo za timu ya taifa ya Kenya zinaweza kuhamishiwa nchini Uganda au Tanzania. CAF ilitaja ukiukwaji mwingi, ikiwa ni pamoja na kukanyagana kulikosababishwa na kuingia bila kibali, mashabiki kuwasha moto, pikipiki kupita katikati ya watu, na kushambuliwa kwa wafanyikazi na wafadhili wa CAF na mlinzi aliye na kandarasi. Matukio ya ziada wakati wa mechi dhidi ya Angola na Morocco yalihusisha mashabiki kuruka vizuizi na kuwasha milipuko ndani ya uwanja. Kwa kujibu, CAF ilisitisha uuzaji wa tikiti kwa michezo yote ya Kasarani, pamoja na mpambano ujao wa Kenya na Zambia. Shirikisho la Soka la Kenya limepigwa faini ya karibu shilingi milioni 2.5 za Kenya kutokana na ukiukaji huo. Kenya sasa imepigwa jumla ya aini ya Sh10.5 milioni tangu kipute cha Kombe la Afrika kwa Wachezaji Wanaoshiriki Ligi za Nyumbani (CHAN 2024) ianze mwezi huu, hali hii ikichochewa na mashabiki kukosa kuzingatia sheria za CAF. Miamba ya soka barani Afrika kama Nigeria, Zambia, DRC, Afrika Kusini zimefungishwa virago na kuyaaga mashindano hayo ya kikanda.
Dondoo za Hapa na Pale
Timu ya soka ya Watanzania iitwayo Kilimanjaro kutoka Sweden imetwaa tena kwa mara ya nne mfululizo ubingwa wa kombe la Bonanza la Serengeti katika michuano iliyofanyika tarehe 15-16 Agosti, 2025, jijini Antwerp, Ubelgiji. Kilimanjaro ilitetea ubingwa wake baada ya kuifunga timu nyingine ya Watanzania kutoka Uingereza iitwayo Leeds Swahili mabao 2-1 kwenye mchezo mkali wa fainali. Magoli ya Kilimanjaro yalifungwa na Feisal Amir na Fryad Sabri huku la Leeds likifungwa na Murtaza Fuad. Hii ni mara ya tatu kwa timu hizi kukutana fainali.
Mbali na hayo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alitunukiwa Nishani ya Heshima ya Juu ya Baraza la Michezo ya Majeshi Duniani (The Grand Cordon) na Makamu wa Rais wa CISM Kanda ya Afrika Meja Jenerali Maikano Abdullahi kutoka Nigeria kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 14 Agosti, 2025. Viongozi pamoja na wageni mbalimbali waliohudhuria hafla hiyo wamempongeza Mama Samia kwa kutunukiwa Nishani ya CISM.

Kwengineko, klabu ya Young Africans SC (Yanga) imetoa ufafanuzi kuhusu mchango wa Shilingi milioni 100 uliotolewa katika Harambee ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) tarehe 12 Agosti 2025, kufuatia mjadala ulioibuka kwenye mitandao ya kijamii na miongoni mwa wanachama ambapo Klabu hiyo imeweka wazi kuwa fedha hizo hazikutoka kwenye akaunti wala mapato ya klabu. Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya klabu hiyo iliyotolewa leo Agosti 14, 2025, fedha hizo zilitolewa na GSM Foundation taasisi inayomilikiwa na mfadhili na mdhamini wa Yanga Ghalib Said Mohammed ambapo Yanga imeeleza kuwa mchango huo ulitolewa na taasisi hiyo kwa niaba yake binafsi na si kama sehemu ya shughuli au maamuzi ya klabu. Taarifa hiyo imefafanua kuwa kwa zaidi ya miaka mitatu, GSM Foundation imekuwa mshirika wa karibu wa Yanga katika kusaidia shughuli za kijamii ndani na nje ya nchi, hivyo uhusiano huo haumaanishi kwamba kila hatua ya mfadhili wao ni ya klabu moja kwa moja. Klabu hiyo imesisitiza kuwa hakukuwa na matumizi ya fedha za wanachama wala mapato ya klabu kwenye mchango huo. Huku hayo yakiarifiwa, Klabu ya Young Africans SC imekanusha taarifa zilizoenea kuwa Rais wake, Mhandisi Hersi Said, amechukua fomu ya kugombea ubunge wa Jimbo la Kongwa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Msemaji wa klabu hiyo, Ally Kamwe, akizungumza na waandishi wa habari mjini Kigali, Rwanda Ijumaa hii, amesisitiza kuwa Hersi hakuchukua fomu katika jimbo hilo wala kuonesha dhamira ya kugombea nafasi hiyo. Awali, vyombo mbalimbali vya habari nchini, viliripoti kwamba jina la Hersi lilikuwa miongoni mwa majina 24 ya makada waliojitokeza kuwania ubunge wa Jimbo la Kongwa, lakini halikupenya katika mchujo wa awali. Kabla ya hapo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeishutumu Klabu ya Yanga kwa kile kinachodaiwa kuwa mchango wa Shilingi milioni 100 kusaidia kampeni za CCM, kikiutaja kama kitendo cha kukiuka kanuni za michezo na kuwagawa wanachama wake. Katika taarifa yake ya Agosti 15, 2025, CHADEMA kupitia Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi Brenda Rupia, imesema maelezo ya Yanga yaliyotolewa Agosti 14, 2025 kwamba fedha hizo zilitolewa na mdhamini wao GSM kupitia taasisi ya GSM Foundation, yanakinzana na kauli ya awali ya Rais wa klabu hiyo, Mhandisi Hersi Said, aliyenukuliwa akisema Yanga imechangia CCM milioni 100 na GSM bilioni 10.

Tukisalia nchini Tanzania, Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), umemthibitisha Wallace Karia kuendelea kuwa Rais wa shirikisho hilo kwa kipindi cha miaka minne ijayo. Hatua ya kumthibitisha imetokana na kuwa mgombea pekee wa nafasi hiyo, hivyo wajumbe wote 76 waliokuwa na sifa ya kupiga kura walinyoosha mikono kumthibitisha kwa wadhifa huo hadi mwaka 2029. Athuman Nyamlani amebaki pia katika nafasi yake ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa TFF.

Mechi za ufunguzi wa Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza na ligi nyinginezo za kimataifa zimeanza kurindima. Klabu ya Arsenal Jumapili iliibana Manchester United na kuizaba bao 1-0 katika uwanja wa Old Trafford kwenye mechi ya marudiano katika mzunguko wa ufunguzi wa EPL. Cha kuvutia zaidi kwa kuanza ligi hii, ni muendelezo wa kampeni ya kutaka utawala wa Kizayuni wa Israel upigwe kadi nyekundu na kufukuzwa kwenye Shirikisho la Soka Duniani FIFA, kwa kuua mamia ya wanasoka na wanamichezo wengine huko Gaza tokeo Oktoba 7, 2023.
………………..TAMATI…………….