Waziri wa Ulinzi: Hakuna anayeweza kuitishia Iran yenye nguvu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i100090-waziri_wa_ulinzi_hakuna_anayeweza_kuitishia_iran_yenye_nguvu
Waziri wa Ulinzi wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu hivi sasa ina nguvu na uwezo mkubwa wa kiulinzi, na kwamba hakuna yeyote anayeweza kulitishia taifa hili.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 19, 2023 08:09 UTC
  • Waziri wa Ulinzi: Hakuna anayeweza kuitishia Iran yenye nguvu

Waziri wa Ulinzi wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu hivi sasa ina nguvu na uwezo mkubwa wa kiulinzi, na kwamba hakuna yeyote anayeweza kulitishia taifa hili.

Brigedia Jenerali Mohammad Reza Ashtiani amesema hayo leo Jumatano pambizoni mwa kikao cha Baraza la Mawaziri hapa mjini Tehran, baada ya Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) kutangaza habari ya kutuma ndege zaidi za kivita na manowari za kijeshi katika eneo la Ghuba ya Uajemi. 

Brigedia Jenerali Ashtiani amesema: Marekani inafuatilia malengo yake, lakini Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kimsingi hivi sasa ipo katika marhala ya nguvu na uwezo mkubwa, na haiwezi kutishwa na yeyote.

Juzi Jumatatu, Pentagon iliagiza kutumwa manowari ya USS Thomas Hudner, na ndege za kivita za F-35 na F-16 katika eneo la Ghuba ya Uajemi, eti kwenda kulinda maslahi ya Marekani na uhuru wa safari za baharini katika eneo.

Akijibu uchokozi huo, Jenerali Ashtiani amesema Jamhuri ya Kiislamu iko imara katika kuimarisha uwezo wake wa kuzuia mashambulizi na kusisitiza kwamba, taifa la Iran hususan vikosi vyake vya ulinzi havimuogopi adui yeyote yule.

Waziri wa Ulinzi wa Iran ameongeza kuwa, Vikosi vya Ulinzi vya nchi hii vina uwezo wa kutosha wa kudhamini usalama wa taifa na wa nchi zote za eneo hili la kistratajia la Asia Magharibi.

Jana Jumanne, Mkuu wa Majeshi ya Iran, Meja Jenerali Mohammad Baqeri alisema kutokana na uwezo endelevu wa kujihami wa Iran, maadui hivi sasa hawazungumzi tena kuhusu 'chaguo la kijeshi' dhidi ya nchi hii.