Raisi: US, nchi za Ulaya zilipanga ghasia za mwaka jana Iran
Rais wa Iran ameikosoa Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya kwa kuratibu machafuko yaliyoshuhudiwa mwaka jana hapa nchini Iran kwa kisingizo cha kifo cha Mahsa Amini.
Rais Ebrahim Raisi alisema hayo jana Jumatatu katika mkutano wake na wanachama wa kamati iliyoundwa kuchunguza ghasia hizo zilizoshuhudiwa katika pembe mbalimbali za Iran mwaka jana.
Sayyid Raisi amesema: Marekani, baadhi ya nchi za Ulaya na maadui wengine wa Iran walilikosea taifa la Iran, kwa kulenga usalama, utulivu, biashara na fikra za watu wetu kwa kupanga na kuchochea ghasia. Hata hivyo watu wetu walizima njama hizo kwa kusimama kidete.
Rais wa Iran amesisitiza kuwa, haki na uadilifu vinafaa kuzingatiwa katika mchakato wote wa uchunguzi wa machafuko hayo yaliyochochewa na kushadidishwa na Wamagharibi.
Vyombo vya habari vya Maghairibi vilichochea ghasia hizo zilizoshuhudiwa hapa Iran kwa kisingizo cha kuaga dunia Mahsa Amini, mwanamke Muirani aliyezirai katika kituo cha polisi na kisha kupoteza maisha wakati akiwa anapata matibabu hospitalini Septemba mwaka jana.
Awali kulikuwa na maandamano ya amani kulalamikia kifo hicho, lakini wapinzani wa mfumo wa Kiislamu waliteka maandamano hayo na kuchochea hujuma dhidi ya maafisa wa usalama na ghasia zilizopelekea kuharibiwa mali za umma.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu Iran ameongeza kuwa, watu wote ambao haki zao zilihujumiwa au waliathirika kwa njia moja au nyingine kutokana na ghasia hizo wanapasawa kulipwa fidia.