Idara ya Mahakama yawalaumu walionyamazia kimya shambulio la kigaidi la Shah Cheragh
Msemaji wa Idara ya Mahakama ya Iran ameyalaumu madola na mashirika yanayodai kutetea haki za binadamu kwa kunyamazia kimya shambulio la kigaidi katika Haram ya Shah Cheragh ya kusini mwa Iran.
Alkhamisi jioni gaidi mmoja mkufurishaji aliingia na silaha katika Haram Takatifu ya Sayyid Ahmad bin Musa (AS) maarufu kwa jina la Shah Cheragh katika mkoa wa Fars wa kusini mwa Iran na kuwafanyatulia risasi kiholela wafanyaziara na wahudumu wa haram hiyo tukufu.
Hujuma hiyo ya kigaidi imepelekea watu wawili kuuawa shahidi na wengine wanane kujeruhiwa. Gaidi aliyehusika na hujuma hiyo alikamatwa mara moja katika operesheni ya maafisa usalama waliokuwa wakilinda eneo hilo.
Shirika la habari la Iran Press limemnukuu Bw. Masoud Setayeshi, Msemaji wa Idara ya Mahakama ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akiesema leo Jumanne mbele ya waandishi wa habari kwamba anawalaumu vikali wale wanaodai kupigania haki za binadamu kwa kunyamazia kimya shambulio hilo la kigaidi.
Amesema: Inasikitisha kuona kitendo cha kigaidi kimepangwa na magaidi wa kimataifa na kufanywa ndani ya Iran lakini husikii sauti yoyote kutokana kwa wanaodai kutetea haki za binadamu ulimwenguni.
Msemaji huyo wa Idara ya Mahakama ya Iran vile vile amesema, idara hiyo inaendelea kuwafuatilia kwa karibu wote waliohusika na waliotoa amri ya kufanyika hujuma hiyo ya kigaidi.
Ikumbukwe pia kuwa, siku ya Jumatano ya tarehe 26 Oktoba 2022, kulifanyika shambulizi jingine la kigaidi kwenye haram hiyo takatifu ya Shah Cheragh iliyopelekea kuuawa shahidi watu 13 wasio na hatia.
Genge la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) lililoundwa na Marekani, ndilo lililotangaza kuhusika na mashambulizi hayo yote mawili ya kigaidi.