Uanachama rasmi wa Iran katika kundi la BRICS; risala na matokeo
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i101512-uanachama_rasmi_wa_iran_katika_kundi_la_brics_risala_na_matokeo
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekubaliwa rasmi na kuwa mwanachama wa BRICS miezi kadhaa tu baada ya kukubaliwa uanachama pia katika Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 26, 2023 10:10 UTC
  • Uanachama rasmi wa Iran katika kundi la BRICS; risala na matokeo

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekubaliwa rasmi na kuwa mwanachama wa BRICS miezi kadhaa tu baada ya kukubaliwa uanachama pia katika Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai.

Historia ya BRICS inarudi nyuma hadi 2001. Nchi nne zenye nguvu za kiuchumi duniani na zenye kuinukia kiuchumi ikiwemo Brazil, Russia, China na India zilipendekeza kuundwa kundi la BRICS. Hatimaye, Kundi la BRIC lilianzishwa rasmi Juni 16, 2009, na kwa kuongezwa kwa Afrika Kusini Septemba 21, 2010, jina lake lilibadilishwa kutoka BRIC hadi BRICS.

Mkutano wa 15 wa kilele wa BRICS ulifanyika kuanzia Jumanne iliyopita hadi Alkhamisi huko Johannesburg nchini Afrika Kusini.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Seyyid Ebrahim Raisi, aliwasili nchini humo Alkhamisi asubuhi kwa mwaliko rasmi wa Cyril Ramaphosa, Rais wa Afrika Kusini kwa minajili ya kushiriki katika mkutano wa kilele wa BRICS. Katika mkutano wake na  waandishi wa habari akiwa pamoja na viongozi wa China, Brazil, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Russia na Waziri Mkuu wa India, Rais wa Afrika Kusini alitangaza kukubali kundi la BRICS uanachama wa Iran, Argentina, Saudi Arabia, Misri, Imarati na Ethiopia katika kundi hilo.

Kujiunga kwa Iran katika kundi la BRICS kunaweza kutajwa kuwa mafanikio ya tatu muhimu ya serikali ya awamu ya 13 ya Iran katika sera za kigeni. Kukubaliwa kujiunga na Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai na kurejesha uhusiano na Saudi Arabia yalikuwa mafanikio mengine mawili ya serikali ya Rais Ebrahim Raisi katika uga wa sera za kigeni.

 

BRICS ni muungano wa kuvuka bara, na nchi kutoka mabara ya Asia, Afrika na Ulaya, ambayo kila moja ni nguvu ya kiuchumi ya dunia inayochomoza ya dunia, na vilevile wanachama wake wawili, yaani Russia na China, ni wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambao wana haki ya kura ya turufu, na hili ni jambo ambalo linaongeza umuhimu kundi hili.

Ujumbe muhimu wa Iran kujiunga na Shanghai na BRICS ni kwamba sera za kuitenga Iran katika mfumo wa dunia si tu kwamba zimefeli, bali kivitendo kumekuwa na mwamko wa kupokewa suala la kuimarisha uhusiano na Iran hasa kutoka kwa madola makubwa na yanayoinukia kiuchumi.

Hussein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, kujiunga Iran na BRICS kunabatilisha vikwazo na kuharibu mipango ya kuitenga Iran na bila shaka ni fursa ya kupanua uhusiano wa kisiasa na mabadilishano ya kibiashara.

Kadhalika Abdollahian ameandika: Nchi za BRICS zenye wakazi zaidi ya bilioni 3 ambao ni asilimia 40 ya watu wote duniani na zenye eneo lenye mitamraba ambazo sawa na theluthi moja ya dunia, zina uwezo muhimu wa ushirikiano wa pande mbili na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Mkabala na hayo, uwezo wa thamani wa nchi yetu, ikiwa ni pamoja na nafasi ya kijiopolitiki, kistratejia, rasilimali nyingi za nishati, rasilimali watu yenye ujuzi na utaalamu, maendeleo makubwa katika nyanja mbalimbali na uthabiti wa kisiasa ni mambo ambayo yanazingitaiwa na wanachama wa BRICS.

Matokeo muhimu ya uanachama rasmi wa Iran katika kundi la BRICS ni kwamba, kusambaratishwa vikwazo vya Marekani na Ulaya kutawezekana zaidi kuliko hapo kabla. Kazem Jalali, balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Russia ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii: Kukubaliwa uanachama wa Iran katika kundi la BRICS kutaandaa uwanja na mazingira ya maingiliano ya karibu na ya kujenga uaminifu na wanachama na waasisi wake wakuu.

Marais wa Iran na Tanzania wakiwa pambizoni mwa mkutano wa BRICS nchini Afrikka Kusini

 

Ni dhahir shahir kwamba, jambo hili litaandaa fursa mpya katika kuchanua sera za kigeni za Iran na hivyo kuweza kukabiliana na mashinikizo na vikwazo vya madola ya Magharibi.

Moja ya malengo ya BRICS ni kujitenga na sarafu ya dola katika miamala ya biashara ya kimataifa. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ambayo ikiwa na lengo la kufubaza vikwazo vya Marekani, imeliweka katika ajenda zake suala kufanya biashara na sarafu za kitaifa au sarafu zinginezo lakini sio sarafu ya dola, inaweza kunufaika vyema na sera hii ya BRICS.

Mtandao wa habari wa Bloomberg umeandika katika ripoti yake kwamba: Kwa kuzingatia kuwa, biashara nyingi za kimataifa za nishati zinafanyika kwa sarafu ya dola, ustawi wa BRICS utaimarisha uwezo wake wa kukuza biashara kwa matumizi ya sarafu mbadala.