Sep 04, 2023 14:06 UTC
  • Raisi: Mapambano ya nchi za Kiafrika dhidi ya ukoloni ni ishara ya mwamko na kuwa macho

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amepongeza kusimama kidete na mapambano ya nchi za Kiafrika dhidi ya ukoloni na ugaidi, na kuyataja kuwa ni ishara ya mwamko, kuwa macho na utambuzi sahihi wa mahitaji ya zama ya nchi hizo.

Rais Sayyid Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyasema hayo leo Jumatatu katika mazungumzo yake na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Burkina Faso, Bibi Olivia Rouamba aliyeko safarini mjini Tehran. Ameashiria uhusiano mzuri wa Iran na nchi zote za Afrika baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, na utayarifu wa Jamhuri ya Kiislamu kuhamishia tajriba na mafanikio yake kwa nchi marafiki hususan za bara la Afrika.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia amesema kuanzishwa wa Kamisheni ya Pamoja ya Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Iran na Burkina Faso kutakuwa na taathira katika kuharakisha mabadilishano ya uwezo wa pande mbili na kuboresha kiwango cha uhusiano na ushirikiano.

Bibi Olivia Rouamba

Kwa upande wake Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Burkina Faso, Bibi Olivia Rouamba ameeleza kuwa nchi za Kiafrika, ikiwemo Burkina Faso, zimetiwa moyo na muqawama wa Mapinduzi ya Kiislamu dhidi ya ubeberu na kusema: "Ajenda muhimu zaidi ya serikali ya Burkina Faso ni kutia msukumo katika ushirikiano wake na Iran."

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Burkina Faso amesema: Nchi yake ina hamu ya kuimarisha ushirikiano na nchi rafiki ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Tags