Jun 16, 2024 02:39 UTC
  • Serikali ya Sudan yakanusha kuwepo njaa nchini humo

Serikali ya Sudan imekanusha uwezekano wa kutokea baa la njaa nchini humo. Hayo ni kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan.

Katika sehemu moja ya taarifa yake, wizara hiyo imesema: "Serikali ya Sudan inasisitiza kuwa hakuna njaa inayokaribia kutokea humu nchini."

Wizara hiyo imedai pia kuwa, ripoti za Wizara ya Kilimo ya Sudan na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) ni ushahidi wa madai hayo ya serikali ya Khartoum.

Wizara ya Mambo ya Nje wa Sudan pia imesema kuwa, Umoja wa Mataifa unaweza kununua chakula kutoka soko la ndani na maeneo mengine ya uzalishaji chakula nchini humo.

Kuongezeka vita vya uchu wa madaka baina ya majenerali wa kijeshi huko Sudan kimeinakamisha nchi hiyo na kuharibu vibaya mno miundombinu yake.

Mkurugenzi Mkuu wa FAO, Qu Dongyu alisema Jumatatu iliyopita katika hotuba yake kwa mkutano wa shirika hilo kwamba "hatari ya njaa ni ya kweli nchini Sudan," ambapo nusu ya watu wanakabiliwa na viwango vya juu vya uhaba wa chakula.

Kabla ya hapo pia, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) lilikuwa limeonya kwamba vita vinavyoendelea nchini Sudan vitapelekea kuzuka janga kubwa zaidi la njaa nchini Sudan, ambayo raia wake tayari wanateseka kutokana na kuhama makazi yao kwa sababu ya vita.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, nusu ya wakazi wa Sudan wanahitaji msaada wa kibinadamu na ulinzi, na karibu watu milioni 18 wanateseka kwa uhaba mkubwa wa chakula.

Tags