Iran: Tuko tayari kuongoza mkutano wa nchi za Kiislamu kujadili Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i103302-iran_tuko_tayari_kuongoza_mkutano_wa_nchi_za_kiislamu_kujadili_palestina
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu ipo tayari kuwa mwenyeji wa mkutano wa dharura wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC), kwa ajili ya kuzungumzia kadhia ya Palestina.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Oct 10, 2023 10:10 UTC
  • Iran: Tuko tayari kuongoza mkutano wa nchi za Kiislamu kujadili Palestina

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu ipo tayari kuwa mwenyeji wa mkutano wa dharura wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC), kwa ajili ya kuzungumzia kadhia ya Palestina.

Hossein Amir-Abdollahian amesema hayo katika mazungumzo yake ya simu na Hissein Brahim Taha, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) na kusisitiza kuwa, kuungwa mkono taifa la Palestina ni jukumu la mataifa yote ya Kiislamu.

Sanjari na kutoa mwito wa kuitishwa kikao cha dharura cha OIC, Amir-Abdollahian ameeleza bayana kuwa, mataifa ya Kiislamu yana wajibu wa kuchukua hatua za dharura kuwasaidia ndugu zao wa Palestina.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran amekumbusha kuwa, taifa hili daima limekuwa na misimamo ya wazi na madhubuti kuhusu Palestina, na itaendelea kuunga mkono na kutetea haki za wananchi madhulumu wa Palestina.

Ukatili wa wanajeshi wa Israel katika Ukanda wa Gaza

Kwa upande wake, Hissein Brahim Taha, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) mbali na kulaani mashambulizi ya kinyama ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina, ametoa mwito kwa kuimarishwa ushirikiano miongoni mwa nchi za Kiislamu ili kwa pamoja zitoe jibu la pamoja dhidi ya Israel.

Kadhalika amepongeza mpango wa Iran wa kuwa mwenyeji wa kikao maalumu cha mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu, cha kujadilii matukio yanayoendelea kushuhudiwa katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.