Iran yakanusha madai ya kuendelea kuzuiliwa fedha zake zilizoachiwa
Ofisi ya Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa imekadhibisha ripoti iliyochapishwa na gazeti la Washington Post kuwa, Marekani na Qatar zimeafikiana kuzuia fedha za Iran zilizoachiwa hivi karibuni, ambazo zilikuwa zinashikiliwa nchini Korea Kusini kutokana na vikwazo.
Taarifa ya jana Alkhamisi ya ofisi hiyo ya kidiplomasia ya Iran mjini New York imeeleza bayana kuwa, ripoti hiyo ya Washington Post haina mashiko wala ukweli wowote.
Mapema jana, gazeti hilo lilimnukuu Wally Adeyemo, Naibu Waziri wa Fedha wa Marekani akidai kuwa Doha na Washington zimekubaliana kuizuia Iran isichukue fedha hizo, eti baada ya Harakati ya Palestina ya Hamas kufanya shambulizi la kushtukiza dhidi ya Israel.
Ofisi ya Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa imebainisha kuwa, madai hayo ya Washington Post ya kufikiwa makubaliano baina ya Marekani na Qatar ya kuzuilia dola bilioni 6 fedha za Iran, hayatakuwa na matokeo mengine ghairi ya kulipotezea itibari gazeti hilo.
Qatar imekuwa mpatanishi katika mazungumzo yaliyopelekea makubaliano ya kubadilishana wafungwa kati ya Iran na Marekani ambayo yalitangazwa rasmi tarehe 10 Agosti. Makubaliano hayo yanahusisha kuachiliwa kwa wafungwa watano kutoka kila upande pamoja na kuachiliwa dola bilioni 6 za Iran ambazo zilikuwa zinashikiliwa tangu 2018 katika benki mbili nchini Korea Kusini kwa sababu ya vikwazo vya Marekani.
Mchakato wa kuhamisha fedha hizo ulichukua zaidi ya mwezi mmoja hasa kwa sababu kulikuwa na kiwango maalumu cha fedha hizo za Iran ambazo zingeweza kuhamishwa kila siku kutoka benki za Korea Kusini.
Jana Alkhamisi pia, shirika la habari la Nour News lenye mfungamano na Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran lilipuuzilia mbali ripoti hiyo ya Washington Post na kusisitiza kuwa: Hakuna mabadiliko yoyote kuhusu suala la Iran kufikia fedha zake za kigeni katika benki za Qatar, na makubaliano (ya kuachia fedha hizo) yangali yanatekelezwa.