Abdollahian: Sera za Marekani zinachochea moto wa vita Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i103600-abdollahian_sera_za_marekani_zinachochea_moto_wa_vita_gaza
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema sera haribifu za Washington na uungaji mkono wake kwa hatua ya utawala wa Kizayuni ya kuwashambulia raia katika Ukanda wa Gaza ndiyo sababu kuu ya kushadidi na kupanuka vita katika eneo hilo la pwani ambalo liko chini ya mzingiro.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 17, 2023 10:05 UTC
  • Abdollahian: Sera za Marekani zinachochea moto wa vita Gaza

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema sera haribifu za Washington na uungaji mkono wake kwa hatua ya utawala wa Kizayuni ya kuwashambulia raia katika Ukanda wa Gaza ndiyo sababu kuu ya kushadidi na kupanuka vita katika eneo hilo la pwani ambalo liko chini ya mzingiro.

Hossein Amir-Abdollahian,  Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema hayo katika mazungumzo yake kwa njia ya simu na Josep Borrell, Mkuu wa Sera za Kigeni za Umoja wa Ulaya na kubainisha kwamba, "Kwa bahati mbaya, raia baina ya 300 na 700 wanauawa kila siku Gaza. "

Abdollahian ameeleza bayana kuwa, kutokana na mzingiro na kufungwa korido zote za kibinadamu katika eneo la Ukanda wa Gaza linalokaliwa kwa mabavu, haiwezekani kutuma chakula na dawa kwa wakazi wa ukanda huo.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran amesisitiza kuwa, iwapo jinai za Israel zitaachwa ziendelee bila ya kuchukuliwa hatua za haraka za kuzizuia, basi dunia itashuhudia kuanza medani mpya za vita vya silaha dhidi ya utawala wa Kizayuni.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amelikosoa vikali jeshi katili la utawala wa Kizayuni kwa kuendelea kushambulia nyumba na makazi ya raia huko Gaza kutokana na kushindwa kwenye medani za vita.

Hujuma za kikatili za Israel dhidi ya Gaza

Josep Borrell, Mkuu wa Sera za Kigeni za Umoja wa Ulaya kwa upande wake amesema kupanuka taharuki katika eneo ni hatari kwa usalama na kusisitiza kuwa, kuna haja kwa pande zote husika kujizuia na kutochukua hatua za kushadidisha hali mambo.

Amedai kuwa, Umoja wa Ulaya utaendelea kuufanya juhudi za kuhitimisha vita na kueleza kuwa, EU inasisitizia udharura wa kufungulia njia za kibinadamu ili kuwasaidia wakazi wa eneo la Gaza.

Kadhalika Mkuu wa Sera za Kigeni za Umoja wa Ulaya amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina nafasi muhimu katika kupunguza taharuki na mizozo katika eneo.