Oct 22, 2023 15:00 UTC
  • Amir Abdollahian na Pandor, Tehran
    Amir Abdollahian na Pandor, Tehran

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema katika mkutano wake na waandishi wa habari pamoja na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Afrika Kusini kwamba: Hii leo dunia inashuhudia jinai zinazofanywa na utawala wa kibaguzi na muuaji wa watoto wachanga dhidi ya watu wa Gaza.

Amir Abdollahian ameyasema hayo leo mjini Tehran akiwa pamoja na mwenzake wa Afrika Kusini, Naledi Pandor, anayeongoza ujumbe wa serikali ya Pretoria hapa nchini

 Baada ya mazungumzo ya pande hizo mbili Amir Abdollahian amewaambia waandishi wa habari, kwamba: Leo, pamoja na masuala ya pande mbili, tumejadili pia masuala yanayoendelea Ukanda wa Gaza, na tunaishukuru Afrika Kusini kwa nafasi yake katika kuwatetea watu wa Palestina na mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi wa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema katika kikao hicho kwamba: "Kwa mwaliko wa Rais wa Afrika Kusini, Rais wa Iran, Sayyid Ebrahim Raisi atazuru Afrika Kusini, na katika safari hiyo, hati za mwisho zilizokubaliwa kati ya taasisi za pande mbili, zitatiwa saini na Marais wa nchi."

Amir Abdollahian ameashiria yanayojiri katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu ya Palestina na kusema: Rais Joe Biden wa Marekani amekwenda Tel Aviv kwa kukurupuka na kuutetea utawala unaolenga raia, hospitali na vituo vya makazi, na ametangaza rasmi kuwa atatuma mamia ya ndege za kivita kuwaua watu wa Gaza, kisha anatoa matamshi ya kejeli akisema kwamba, Marekani itapeleka malori ishirini huko Gaza kwa ajili ya misaada ya kibinadamu!

Watoto wa Palestina wanauawa kwa silaha za Marekani

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran ameongeza kuwa: Leo Marekani imeingia katika vita vya wakala dhidi ya watu wa Gaza, na ni lazima isemwe kwamba eneo hili ni pipa la baruti, na mahesabu yoyote yasiyo sahihi, mauaji ya halaiki na kuwalazimisha watu wa Gaza kuhama makazi yao kunaweza kuwa na matokeo mabaya kwa eneo la Magharibi mwa Asia na kwa wachochezi wa vita.

Amir Abdollahian amesisitiza kuwa: Tunaionya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel kwamba iwapo hawatasimamisha mara moja jinai dhidi ya binadamu huko Gaza, kuna uwezekano wa kutokea lolote, wakati wowote; wakati huo udhibiti wa eneo hilo utatoweka na moshi utafuka na kufika machoni mwa watu wanaochochea vita

Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini pia amesema katika mkutano huo kuwa: Wapalestina wananyimwa haki za binadamu na ardhi yao inakaliwa kwa mabavu.

Tags