Rais wa Iran: Kuendelea kwa mauaji ya Wapalestina kutaathiri ulimwengu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i104468-rais_wa_iran_kuendelea_kwa_mauaji_ya_wapalestina_kutaathiri_ulimwengu
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Tehran inaunga mkono juhudi za pamoja za kimataifa kwa ajili ya usitishaji vita mara moja, kuondoa mzingiro na kutoa misaada kwa watu wanaodhulumiwa wa Ghaza na kusisitiza kuwa: Mauaji ya watu wa Palestina yameyakasirisha mataifa yote huru duniani, na kuendelea kwa mauaji haya kutakuwa na matokeo mabaya hadi nje ya kanda ya Magharibi mwa Asia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 07, 2023 04:47 UTC
  • Rais wa Iran: Kuendelea kwa mauaji ya Wapalestina kutaathiri ulimwengu

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Tehran inaunga mkono juhudi za pamoja za kimataifa kwa ajili ya usitishaji vita mara moja, kuondoa mzingiro na kutoa misaada kwa watu wanaodhulumiwa wa Ghaza na kusisitiza kuwa: Mauaji ya watu wa Palestina yameyakasirisha mataifa yote huru duniani, na kuendelea kwa mauaji haya kutakuwa na matokeo mabaya hadi nje ya kanda ya Magharibi mwa Asia.

Sayyid Ebrahim Raisi, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliyasema hayo jioni ya jana Jumatatu katika mazungumzo yake ya simu na Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi na kusema kuwa, mauaji dhidi ya wanawake na watoto wanaodhulumiwa na wasio na hatia, mashambulizi dhidi ya hospitali, shule, misikiti na makanisa na maeneo ya makazi yanalaaniwa wanadamu wote wala hayakubaliki.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu amesema: Makundi ya muqawama ya Palestina yana haki halali ya kukabiliana na uvamizi wa utawala ghasibu wa Israel, na nchi zote zinapaswa kuunga mkono harakati za taifa la Palestina za kupigania uhuru na ukombozi kutoka kwenye dhulma na ukandamizaji.

Raisi Ebrahim Raisi ameitaja operesheni ya kushtukiza ya hivi karibuni ya wanamapambano wa wa Kiislamu wa Palestina kuwa ni jibu la halali kwa sera na jinai za utawala wa Kizayuni, kuporwa na kukalia kwa mabavu ardhi ya Wapalestina, kuua watoto na wanawake na kudhalilisha matukufu ya taifa la Palestina. Amehoji kwa kusema: Inakuwaje kwamba mapambano ya nchi za Ulaya dhidi ya Ujerumani ya Kinazi yanatambuliwa kuwa ni kitendo cha kupongezwa na cha kishujaa, lakini mapambano ya taifa la Palestina dhidi ya utawala unaoua watoto na mtendajinai wa Kizayuni yanalaaniwa na kukemewa!?

Watoto wa Gaza waliouawa kwa mashambulizi ya Israel

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameitaja Marekani kuwa ni mshirika mkuu wa Wazayuni katika jinai hizo kutokana na himaya na uungaji mkono wake kamili wa kifedha, silaha na kijasusi kwa utawala wa Kizayuni wa Israel na vilevile kura yake ya turufu dhidi ya maazimio ya Baraza la Usalama yaliyotaka kukomesha mashambulizi ya Israel huko Gaza.

Vilevile ameashiria mienendo miovu ya nchi za Magharibi katika kuwasilisha picha potofu na isiyo sahihi kuhusu matukio ya Gaza ili kuzishawishi nchi nyingine zikubliane na njama ya kulihamisha kwa lazima taifa la Palestina kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi, na kusema: Mauaji ya umati ya watu wa Gaza ndio uhalifu mkubwa zaidi dhidi ya binadamu katika karne ya 21, ambao lazima ukomeshwe mara moja.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi, pia ameelezea wasiwasi wake kuhusu hali mbaya ya wakazi wa Ukanda wa Gaza kutokana na mashambulizi ya utawala wa Israel, na kupongeza misimamo ya Rais wa Iran ya kuunga mkono na kubainisha matukio ya kweli na halisi ya Palestina.

Waziri Mkuu wa India amesema: Hii leo, kila mtu ana wajibu wa kukomesha mauaji ya wanawake na watoto huko Gaza na kufanya kila awezalo kwa ajili ya kufikisha misada kwa waathirika hao.