Iran yataka Waislamu waungane kukabiliana na ugaidi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i10645-iran_yataka_waislamu_waungane_kukabiliana_na_ugaidi
Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran Mohammad Javad Zarif amelaani vikali msururu wa hujuma za kigaidi nchini Saudi Arabia katika Mji Mtakatifu wa Madina na miji ya Qatif na Jeddah.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 05, 2016 09:09 UTC
  • Iran yataka Waislamu waungane kukabiliana na ugaidi

Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran Mohammad Javad Zarif amelaani vikali msururu wa hujuma za kigaidi nchini Saudi Arabia katika Mji Mtakatifu wa Madina na miji ya Qatif na Jeddah.

Zarif amesema kuna haja ya mataifa ya Waislamu kuungana kwani hiyo ndio njia pekee ya kukabiliana na ugaidi katika eneo la Mashariki ya Kati.

Katika ujumbe aliotuma kwa njia ya Twitter mapema Jumanne, Zarif alisema: "Hakuna tena mistari myekundu kwa magaidi. Masunni na Mashia wasiposimama pamoja wataendelea kuwa waathirika wa ugaidi."

Ujumbe huo wa Zarif umekuja baada ya mashambulizi ya kigaidi yaliyofanyika jana katika miji mitatu tafauti nchini Saudi Arabia likiwemo shambulizi lililotokea karibu na Msikiti wa Mtume SAW katika mji mtakatifu wa Madina ambapo askari wanne waliuawa na gaidi aliyetekeleza hujuma.

Magaidi pia walishambulia msikiti wa Waislamu wa madhehebu ya Shia katika mji wa Qatif huko mashariki mwa Saudia ambapo watu watatu waliuawa akiwemo gaidi aliyetekeleza shambulizi hilo.

Mapema jana Jumatatu pia gaidi moja alipoteza maisha alipojirupua nje ya ubalozi mdogo wa Marekani katika mji wa Jeddah.

Maafisa wa serikali ya Saudia wamesema mshambuliaji wa Jeddah alikuwa raia wa Pakistan aliyetambuliwa kama Abdullah Qalzar Khan aliykuwa akiishi Saudia na familia yake.