Jan 08, 2024 12:11 UTC
  • Kukwepa uwajibikaji na kimya cha Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa kuhusiana na jinai za utawala wa Kizayuni huko Gaza

Katika kuendeleza misimamo inayozusha mizozo ya nchi za Magharibi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa amepuuza jinai zinazotekelezwa na utawala wa Kizayuni huko Gaza na kudai kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inapaswa kukomesha vitendo vyake vinavyovurunga amani na uthabiti wa eneo.

Baada ya mazungumzo yake ya simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amirabdollahian,  Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Catherine Colonna, aliandika kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba amewasilisha ujumbe wa wazi kwa mwenzake wa Iran kwamba hatari ya kuenea moto wa vita wa kieneo ulikuwa haujawahi kufukia kiwango hiki hadi sasa na kuwa Iran na makundi waitifaki wake  lazima waache mara moja vitendo vyao vya kuzusha ghasia na vita katika eneo.

Madai na tuhuma hizo za Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa yanatolewa katika hali ambayo Amir Abdollahian amesisitiza katika mazungumzo hayo ya simu juu ya kusimamishwa mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni huko Gaza. Hii si mara ya kwanza katika kipindi cha siku za hivi karibuni kwa viongozi wa nchi za Magharibi kupuuza jitihada na uungaji mkono Iran kwa usitishwa vita huko Gaza na kutoa madai ya uwongo na ya kuzihadaa fikra za waliowengi kuhusiana na suala hilo.

Tangu kuanza operesheni ya kimbunga cha Al-Aqsa  tarehe 7 Oktoba 2023 hadi leo, Marekani na nchi nyingine za Magharibi zimekuwa zikiuunga mkono wazi wazi utawala wa Kizayuni na hivyo kuzuia kupatikana amani na utulivu huko Gaza.

Machungu wanayopitia watoto wa Gaza

Marekani na Uingereza, ni miongoni mwa nchi ambazo zimekuwa zikipinga kupasishwa maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ya kusitisha vita huko Gaza, na kinyume na madai ya uongo ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa ikitilia mkazo haja ya kukomeshwa mapigano  huko Gaza.

Serikali ya Ufaransa, hivi sasa na katika miaka ya hivi karibuni, daima imekuwa miongoni mwa waungaji mkono muhimu wa utawala wa Kizayuni ambapo imekuwa ikitoa uungaji mkono usio na masharti wa kifedha na silaha kwa Wazayuni makatili.

Ufaransa, Marekani na Uingereza zikiwa nchi zenye kura ya "veto" katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, hazijaonyesha nia yoyote ya kuchukua hatua ya kuwatetea wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina wala kusimamisha uvamizi na jinai za utawala wa Kizayuni katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu. Lakini katika upande wa pili,  viongozi wa Magharibi wamekuwa wakichukua misimamo ya wazi na iliyo dhidi ya muqawama halali wa watu wa Palestina katika uwanja huo.

Majanga wanayopitia kila siku wakazi wavumilivu wa Ukanda wa Gaza

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, amekiri kuhusu uwezo na nguvu ya makundi shujaa ya muqawama ya Palestina na kudai kwamba itachukua miaka 10 ili kuiangamiza Hamas.

Misimamo ya viongozi wa Magharibi katika siku za hivi karibuni inaashiria kutambua kwao nguvu na uwezo wa makundi ya muqawama na vijana wa Kipalestina ambao wameushangaza utawala wa Kizayuni na waitifaki wake hao kutokana na harakati  na kukabiliana kwao vilivyo na kupelekea Wazayuni na marafiki wao kukiri kushindwa tathmini yao kuhusiana na nguvu ya makundi ya mapambano ya Kipalestina.

Maneno ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa pia ni jitihada za kuhadaa maoni ya waliowengi kimataifa ili kuhalalisha athari mbaya za uingiliaji kati wa Marekani na serikali za Magharibi katika matukio ya eneo la Asia Magharibi.

Wataalamu na wachambuzi huru wa Magharibi daima wamekuwa wakisisitiza kuwa, suluhisho la kupatikana uthabiti na amani katika eneo hili ni Marekani na waitifaki wake kujiepusha na kuingilia masuala ya eneo na kusimamisha uungaji mkono wao wa silaha na kifedha kwa utawala wa jibaguzi wa Israel.

 

Tags