Mar 05, 2024 05:14 UTC
  • Uchaguzi wa Iran ni ishara ya umuhimu wa masanduku ya kura na ushiriki wa wananchi

Kuhesabiwa kura za uchaguzi wa Awamu ya 12 ya Majlisi ya Ushauri wa Kiisalmu (Bunge la Iran) na uchaguzi wa Awamu ya Sita ya Baraza la Wanazuoni Wataalamu wanaomchagua Kiongozi Muadhamu kumemalizika kufuatia kushiriki kwa wingi wananchi katika duru hii ya uchaguzi.

Siku ya Ijumaa, Machi 1, 2024, wananchi wa Iran walijitokeza kwa wingi katika vituo mbalimbali vya kupigia kura kote nchini na kama ilivyokuwa katika chaguzi za miaka iliyopita, kwa mara nyingine tena Wairani waliutangazia ulimwengu umuhimu wa ushiriki wa kisiasa na kuamini masanduku ya kupigia kura katika kuwachagua viongozi wao.

Uchaguzi wa Bunge na ule wa Baraza la Wataalamu wa Uongozi wa kipindi hiki pia ulikuwa na sifa ambazo zilitofautiana na chaguzi zilizopita.

Kuwepo orodha mbalimbali za wagombea, na mirengo mipya ya kisiasa hasa katika miji mikubwa ni miongoni mwa mambo yaliyosababisha ushindani mkubwa katika uchaguzi baina ya wagombea jambo ambalo lilipokelewa vizuri na wananchi kwani walikuwa na machaguo ya kutosha. Kutokana na hali hiyo zoezi la upigaji kura liliongezwa muda hadi saa sita usiku wakati muda rasmi wa upigaji kura ulikuwa kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa kumi na mbili jioni.

Zoezi la kuhesabu kura limekamilika ambapo uchaguzi katika baadhi ya miji umeingia katika duru ya pili kutokana na ushindani mkali uliokuwepo.

Uchaguzi wa tarehe 1 Machi (12 Esfand 1402) umeonyesha hamu ya mamilioni ya Wairani ya kushiriki katika mchakato wa kisiasa nchini na imani ya wananchi kwa zoezi la upigaji kura.

Idadi ya ushiriki wa watu katika uchaguzi wa Ijumaa imetangazwa kuwa asilimia 41 ambayo ni sawa na wapiga kura milioni 25.
Katika kipindi hiki cha uchaguzi, vyombo vya habari hasimu vya nchi za Magharibi na baadhi ya mitandao yenye mfungamano na Marekani pamoja na utawala wa Kizayuni wa Israel nje ya Iran vilijaribu kueneza propaganda za upotoshaji ili ushiriki wa wananchi katika zoezi la upigaji kura uwe mdogo.
Propaganda hizo za upotoshaji ziliendelea hadi siku ya uchaguzi, lakini kujitokeza kwa wingi wananchi kwa mara nyingine kumesambaratisha propaganda hizo za maadui dhidi ya Iran.
Mchakato wa kueneza habari hasi ungali unaendelea katika vyombo hivyo vya habari vya maadui hata baada ya uchaguzi, kwa lengo la kudai kuwa mahudhurio ya wananchi kwenye vituo vya kupigia kura yalikuwa madogo.
Hii ni licha ya ukweli kwamba ripoti mubashara za televisheni na maelfu ya picha kutoka maeneo tofauti ya kupigia kura zilionyesha ushirikki mkubwa wa wananchi. Hivyo hakuna hata chembe ya shaka kuwa hakuna ukweli wowote katika propaganda za maadui hao wa Iran.

Uchaguzi wa Ijumaa, kama chaguzi nyingine zilizofanyika Iran miaka ya nyuma, ulikuwa na athari muhimu na ya kimsingi, ambayo ni uwepo mkubwa na ulioenea wa watu kwenye vituo vya kupigia kura.
Mirengo ya kisiasa nchini pia ilichangia pakubwa katika kuwavutia wananchi kushiriki katika zoezi la kupigia kura kwa kuwasilisha orodha mbali mbali.

Sanduku la kura likitayarishwa kwa ajili ya zoezi la kuhesabu kura

Pamoja na kuwa idadi ya wapiga kura imetangazwa rasmi kuwa ni asilimia 41 lakini vyombo vya habari vya Magharibi vingali vinakariri na kurudiarudia kelele za propaganda wakati ukweli ni kuwa katika nchi nyingi za Magharibi idadi ya wanaojitokeza kupiga kura huwa ndogo sana.

Kushiriki kwa wingi wananchi wa Iran katika uchaguzi siku ya Ijumaa ni jambo ambalo limesambaratisha propaganda hizo zisizo na msingi za serikali za Magharibi hasa Marekani na vyombo vyao vya habari. Ni wazi kuwa propaganda hizo potovu hazikuathiri ushiriki mkubwa wa kisiasa wa wananchi katika uchaguzi ambao ni muhimu katika kuamua hatima ya kisiasa ya nchi.