Mar 07, 2024 09:48 UTC
  • Wagonjwa wa ngozi ya kipepeo (EB), waathiriwa wa vikwazo vya Marekani

Jumatano ya jana, Mahakama ya Hata ya Uhusiano wa Kimataifa ya Tehran iliamuru kukamatwa shehena ya mafuta ya Marekani katika maji ya Ghuba ya Uajemi, na shehena ya meli hiyo sasa imekamatwa na vyombo husika vya Iran.

Taarifa iliyotolewa na Mahakama ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesema kuwa, kufuatia vikwazo vilivyowekwa na nchi za Magharibi hususan Marekani vilivyopelekea kuzuiwa uuzwaji wa dawa za kampuni ya Sweden zinazohitajika kwa ajili ya waathiriwa wa ugonjwa wa ngozi wa Epidermolysis Bullosa (EB) nchini Iran suala ambalo limesababisha hali mbaya ya kimwili na kiroho kwa waathirika, wagonjwa wa Epidermolysis Bullosa (EB) waliwasilisha mashtaka dhidi ya Marekani katika Mahakama ya Haki ya Mahusiano ya Kimataifa (Tawi la 55) mjini Tehran.

Kwa ufuatiliaji wa kisheria uliofanywa na wakili wa kesi hiyo, hatimaye Mahakama ya Haki ya Uhusiano wa Kimataifa (Tawi la 55) la Tehran iliamuru kukamatwa kwa shehena ya mafuta ya meli ya ADVANTAGE SWEET katika maji ya Ghuba ya Uajemi, na shehena ya meli hiyo ikakamatwa. Thamani ya shehena hiyo ya mafuta inakadiriwa kuwa zaidi ya dola milioni 50. 

Meli ya mafuta ya ADVANTAGE SWEET

Wakili wa waathirika wa ugonjwa wa ngozi wa Epidermolysis Bullosa (EB) ameeleza kuwa vikwazo vya Marekani vimeilazimisha kampuni ya Sweden kuacha kuuza dawa zinazohitajiwa na wagonjwa hao wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Katika miaka ya hivi karibuni, maafisa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wametahadharisha mara kwa mara kuhusu athari mbaya za vikwazo vya upande mmoja na haramu vya Marekani kwa afya za watu wakiwemo baadhi ya wagonjwa nchini Iran na kusisitiza kuwa, vikwazo hivyo vinasababisha vifo vya wagonjwa kila siku.

Wamagharibi, hasa Marekani, wanadai kuwa dawa na vifaatiba haviko katika orodha ya vikwazo vyao. Kwa mfano tu, akizungumzia tukio la kukamatwa shehena ya meli ya mafuta ya Marekani katika Ghuba ya Uajemi, Matthew Miller, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kwa mara nyingine tena amedai kuwa: Vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran havijawahi kujumuisha dawa. Hii ni licha ya kwamba, vikwazo vya kibenki na matatizo yaliyotokana na kuhawilisha fedha za Iran yamefanya kuwa vigumu na wakati mwingine muhali kupata dawa kwa watu wanaosumbuliwa na magonjwa maalumu na sugu. Matokeo ya vikwazo hivyo ni tishio kwa maisha ya makumi ya maelfu ya wagonjwa, wakiwemo wagonjwa wa ngozi ya kipepeo (EB) pamoja na wale wanaougua thalassemia na saratani nchini Iran.

Kwa hakika, licha ya madai ya Marekani kwamba hakuna vikwazo kwa vifaa vya matibabu na dawa, benki, taasisi na makampuni mengi yamekuwa na tahadhari kubwa katika kufanya biashara na Iran kwa kuhofia uwezekano wa kuadhibiwa na Marekani. Kwa msingi huo, kampuni ya Sweden "Molnlycke" imekataa kutuma bandeji za matibabu kwa wagonjwa wa ngozi ya kipepeo (EB) nchini Iran kutokana na vikwazo vya Marekani. Ni vyyema kuashiria hapa kuwa, karibu wagonjwa 1200 wa ugonjwa wa ngozi wa Epidermolysis Bullosa (EB) nchini Iran wanahitaji haraka bandeji hizo za matibabu.

Athari mbaya za vikwazo vya nchi za Magharibi hasa Marekani dhidi ya Iran haziwaathiri wagonjwa wa ngozi ya kipepeo peke yao, bali hata wagonjwa wa thalassemia na watu wengine wenye magonjwa maalumu pia wako katika hatari ya kupoteza maisha kutokana na vikwazo hivyo. Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, wagonjwa wa thalassemia wamekatiwa dawa wanazohitaji kwa ajili ya matibabu, zaidi ya wagonjwa 670 wamefariki dunia na wagonjwa wengine zaidi ya elfu 10 wamepata madhara makubwa. Haya yote yanaonesha kuwa, vikwazo vya Marekani pia vimetumika katika uwanja wa dawa na matibabu na vimekuwa na athari mbaya kwa wagonjwa hapa nchini. 

Hadi sasa, maripota wa Umoja wa Mataifa wametoa ripoti kadhaa zinazoonesha tabia na mwenendo huo unaokiuka haki za binadamu wa Wamagharibi.

Alena Dohan

Akizungumzia athari mbaya za hatua za upande mmoja zinazovunja haki za binadamu, Alena Dohan, Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa alisisitiza wakati wa safari yake nchini Iran kwamba: "Vikwazo vina taathira kubwa katika mfumo wa afya. Kitu kilichoacha hisia ya kudumu kwangu ni athari mbaya za vikwazo kwenye mfumo wa afya. Nimezungumza na wagonjwa wa dharura na wale wanaougua magonjwa ya kurithi na saratani; Matokeo ni kwamba dawa zinazofaa hazipatikani."