Apr 14, 2024 10:40 UTC
  • Hatua ya kijeshi ya Iran dhidi ya  utawala wa Kizayuni; mfano halisi wa

Katika kujibu shambulio la utawala wa Kizayuni dhidi ya ubalozi mdogo wa Iran huko Damascus, mji mkuu wa Syria, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alfajiri ya Jumapili ya leo tarehe 14 April 2024 imefanya mashambulizi ya moja kwa moja ya ndege zisizo na rubani na makombora katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel).

Jioni ya tarehe 1 Aprili 2024, utawala wa Kizayuni ulishambulia ubalozi mdogo wa Iran huko Damascus na kupelekea kuuawa shahidi washauri saba wakuu wa kijeshi wa Iran. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na ambaye pia ni Amiri Jeshi Mkuu alikitaja kitendo hicho cha Tel Aviv kuwa ni shambulio dhidi ya ardhi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusisitiza kuwa, utawala wa Kizayuni utaadhibiwa. Katika kipindi cha miaka 45 iliyopita, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikishambuliwa moja kwa moja ua kwa njia isiyo ya moja kwa moja, lakini ilifadhilisha kuwa na subira ya kistratejia katika kukabiliana na mashambulizi hayo, ili kujiepusha kuingia katika vita za aina yoyote ile kutokana msimamo wake wa kulinda amani na usalama wa eneo. Kilichofanywa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran leo ni hatua ya "kuiadhibu" Israel na ni katika hatua ya "kujitetea halali" kwa mujibu wa  kifungu cha 51 cha Hati ya Umoja wa Mataifa. Amir Saeed Iravani, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa, Jumamosi usiku, alisisitiza katika barua kwa Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, pamoja na Vanessa Frazier, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Malta, ambaye nchi yake imechukua uenyekiti wa muda wa Baraza la Usalama mwezi huu wa Aprili kuwa: Hatua ya kijeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni haki yake ya kimsingi ya kujilinda, ambayo imeelezwa wazi chini ya Ibara ya 51 ya Hati ya Umoja wa Mataifa na katika kukabiliana na uchokozi wa kijeshi wa mara kwa mara wa utawala wa Israel, hasa mashambulizi ya kijeshi ya utawala huo mnamo Aprili 1, 2024, ambayo ilikuwa kinyume kabisa cha kifungu cha 2 ibara ya 4 ya hatia hiyo.

Utawala wa Kizayuni, kwa uungaji mkono  wa Marekani, unadai kuwa mauaji ya halaiki huko Gaza ni ya kujilinda kwa sababu ulikabiliwa na operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa tarehe 7 Oktoba. Kutolewa madai ya kujilinda katika kukabiliana na mauaji ya kimbari huko Gaza ni madai ya uwongo yanayotolewa katika kuhalalisha  jinai zake dhidi ya wakaazi wa Gaza, kwa sababu wananchi wa Palestina hususan wa Ukanda wa Gaza wamekuwa wakikabiliwa na mashambulizi ya kikatili ya utawala wa Kizayuni kwa zaidi ya miongo 7, na operesheni ya Kimbunga cha  al-Aqsa ni mfano wazi wa harakati ya kujitetea halali huko Gaza katika kukabiliana na jinai hizo. Hatua ya kijeshi ya jana usiku ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran  ilikuwa ya kujilinda halali dhidi ya mashambulizi ya utawala wa Kizayuni katika ubalozi  mdogo wa Iran mjini Damascus.

Wairani wakifurahia na kuunga mkono shambulio la Iran dhidi ya utawala haramu wa Israel

Jambo la pili ni kuwa hatua madhubuti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran dhidi ya utawala wa Kizayuni imechukuliwa kutokana na misimamo dhaifu ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa au kutokuwa na uwezo baraza hilo wa kulaani mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya jengo la ubalozi mdogo wa Iran nchini Syria. Kutochukua hatua Baraza la Usalama na hata uungaji mkono wa baadhi ya wajumbe wa baraza hilo hususan Marekani kwa utawala huo wa kigaidi, kumeifanya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuchukua hatua za kijeshi  kwa ajili ya kujilinda dhidi ya utawala wa Israel unaozikalia kwa mabavu ardhi za Palestina.

Amir Saeed Iravani amesema katika muktadha huo: Kwa bahati mbaya, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeshindwa kutekeleza wajibu wake wa kudumisha amani na usalama wa kimataifa na limeruhusu utawala wa Israel kukiuka na kutoheshimu sheria za kimataifa. suala ambalo limezidisha mivutano ya kieneo na kuhatarisha amani na usalama wa kimataifa. 

Jambo la tatu ni kwamba, katika hatua ya kijeshi dhidi ya utawala wa Kizayuni, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haikulenga mtu au sehemu yoyote ya kiraia. Wakati huo huo, utawala wa Kizayuni ulilenga ubalozi wa Iran, ambao unahesabiwa kuwa sehemu yenye kinga ya kidiplomasia, na kwa upande mwingine, kwa takriban miezi 7 umekuwa ukifanya jinai kubwa zaidi dhidi ya raia wa Gaza. 

Jambo la mwisho ni kuwa hatua ya kijeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran dhidi ya utawala wa Kizayuni ni hatua ya kwanza tu ya kulinda  ardhi yake, na iwapo utawala huo utathubutu kuchukua hatua zaidi za kijeshi dhidi ya Iran, basi utakabiliwa na hatua na jibu kali zaidi kutoka Iran.

Tags