Apr 14, 2024 11:12 UTC
  • Rais Raisi: Hatua yoyote ya kifidhuli itakabiliwa na jibu kali zaidi la Iran

Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema iwapo utawala wa Kizayuni wa Israel utafanya harakati yoyote ya kifidhuli utakabiliwa na jibu madhubuti, zito na kali zaidi.

Kwa mujibu wa IRNA, kufuatia jibu lililotolewa na vikosi vya ulinzi vya Iran kwa vitendo vya kichokozi vya utawala wa Kizayuni dhidi ya maslahi ya Jamhuri ya Kiislamu, Seyyed Ebrahim Raisi ameashiria operesheni ya kihistoria, ya nguvu na ushindi iliyotekelezwa na vikosi vya ulinzi vya Iran na akasema, vijana mashujaa na wenye ghera wa taifa la Iran katika Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, kwa mashauriano na ushirikiano na sekta zote za ulinzi na kisiasa, wamefungua ukurasa mpya katika historia ya nguvu na uwezo wa Iran na kutoa somo lenye mazingatio kwa adui Mzayuni.
 
Raisi amesema, kumtia adabu mchokozi ambayo ni ahadi ya kweli aliyotoa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu imetimizwa; na vikosi vya ulinzi vya kujivunia vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa nguvu na uwezo kamili vimelenga kupitia operesheni za mchanganyiko maeneo na vituo vya kijeshi vya utawala wa Kizayuni katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu; na hatua hiyo imechukuliwa kwa kutumia haki halisi iliyonayo Iran ya kujihami kisheria.
Mashamulio ya makombora ya vikosi vya ulinzi vya Iran

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, ujumbe uliotolewa na shambulio la makombora na ndege zisizo na rubani lililofanywa usiku wa kuamkia leo Jumapili na Iran dhidi ya utawala wa Kizayuni, kwa upande wa umma wa Kiislamu ni kuthibitisha nguvu na uwezo na kuzuia hujuma; na kwa upande wa adui ni kumtia hofu na kumdhalilisha na akasema: katika miezi sita iliyopita na hasa katika siku 10 za hivi karibuni, Iran imetumia kila nyenzo na suhula kikanda na kimataifa ili kuizindua jamii ya kimataifa juu ya hatari kubwa ya kutochukuliwa hatua na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya ukanyagaji wa sheria wa mtawalia unaofanywa na utawala wa Kizayuni, lakini kwa masikitiko, Baraza la Usalama liko chini ya satua na ushawishi wa Marekani na baadhi ya waungaji mkono wengine wa utawala bandia wa Israel, na hivyo limeshindwa kutekeleza majukumu yake.

 
Aidha Raisi amesema, "Muqawama" ni msamiati mkuu wa kuhuisha amani na usalama katika eneo na kupinga uvamizi na kila aina ya ugaidi na akasisitiza kwamba kwa mtazamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran chimbuko la mgogoro katika eneo ni mauaji ya kimbari na khulka ya ukatili ya utawala wa Kizayuni.../
 

Tags