Haki za binadamu, fimbo ya siasa za nje za madola ya mabeberu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i11257-haki_za_binadamu_fimbo_ya_siasa_za_nje_za_madola_ya_mabeberu
Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa, haki za binadamu zinatumiwa kama fimbo ya siasa za nje ya madola ya kibeberu na kwamba Umoja wa Mataifa umeshindwa kukabiliana na mashinikizo ya madola hayo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 14, 2016 23:41 UTC
  • Haki za binadamu, fimbo ya siasa za nje za madola ya mabeberu

Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa amesema kuwa, haki za binadamu zinatumiwa kama fimbo ya siasa za nje ya madola ya kibeberu na kwamba Umoja wa Mataifa umeshindwa kukabiliana na mashinikizo ya madola hayo.

Ghulamhussain Dahqani ameliambia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwamba, umoja huo umepatwa na maradhi ya kufanya kazi kwa kutilia maanani maslahi ya kisiasa ya madola makubwa na kwamba mwenendo huo unakwenda kinyume na ule wa shakhsia wakuwba wanaofanya jitihada za kueneza uadilifu na amani na kuhuisha thamani na matukufu ya kibinadamu. Amesema thamani na matukufu hayo yamo katika mafundisho ya Mitume wa Mwenyezi Mungu.

Hotuba ya balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa inaakisi mtazamo wa Jamhuri ya Kiislamu kuhusu haki za binadamu na thamani zake. Hali ya sasa ya dunia inaonesha kuwa, licha ya kupita kipindi cha ukoloni, vita, utumwa na ubaguzi wa rangi lakini kuna baadhi ya pande zinazoendeleza mambo hayo katika suara mpya.

Hali ya haki za binadamu huko Marekani na katika nchi za Ulaya inaonesha kuwa, dunia ya sasa bado iko mbali sana na kipindi timilifu cha thamani za kibinadamu. Mauaji ya kinyama ya watu weusi huko Marekani na kuendelea kubaguliwa na kukandamizwa wananchi kwa msingi wa rangi au dini zao ni kielelezo cha ukweli huo mchungu.

Kama alivyosema mwakilishi wa Iran katika Umoja wa Mataifa, dunia ambayo watu 62 tu wanamiliki utajiri sawa na ule wa nusu ya jamii ya watu wote dunia na asilimia moja tu ya watu wake wanamiliki mali inayozidi ya asilimia 99 iliyobakia ya watu wote duniani, haiwezi kuwa dunia yenye amani, suluhu na uadilifu.

Ukweli ni kuwa siasa na misimamo ya madola ya kibeberu imejaa ukiukaji wa wazi wa haki za binadamu. Uungaji mkono wa madola hayo kwa ugaidi na makundi ya kigaidi, ukiukaji wao wa sheria za kimataifa, kutotekeleza makubaliano ya kuharibu silaha za mauaji ya halaiki na yale ya mazingira na kupuuza haki ya mataifa mbalimbali ya kujiainishia hatima na mustakbali wao ni miongoni mwa mambo yenye taathira mbaya kwa jamii ya dunia ya sasa.

Nchi zinazodai kutetea haki za binadamu zinaitambua hatua yoyote ya kukosoa au kulaani nchi washirika wao zinazotenda jinai za kivita na kuuwa watoto wadogo kuwa ni mstari mwekundu usioweza kuvukwa! Mfano wa wazi wa ukweli huo ni kuondolewa Saudi Arabia na washirika wake katika mashambulizi dhidi ya watu wa Yemen katika orodha ya nchi zinazovunja haki za watoto duniani.

Katika ripoti yake ya hivi karibuni, Umoja wa Mataifa uliiweka Saudia na washirika wake katika orodha ya wakiukaji wakubwa wa haki za watoto wadogo na kusema kuwa, nchi hizo zinahusika na asilimia 60 ya mauaji ya mamia ya watoto wa Yemen. Hata hivyo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon alijitokeza baadaye mbele ya vyombo vya habari na kusema kuwa, ameiondoa Saudi Arabia na washirika wake katika orodha hiyo. Ban Ki-moon alikiri kuwa hatua hiyo imechukuliwa kutokana na mashinikizo ya Marekani na watawala wa Riyadh.

Ni kutokana na mambo kama hayo ndiyo maana mwakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa akasema umoja huo unahitaji mageuzi ili uweze kuhudumia na kuboresha haki za binadamu na thamani na matukufu ya kimsingi kama uadilifu na usawa. Umoja wa Mataifa unapaswa kuwa na uwezo wa kukabiliana na mashinikizo yote ya nchi zinazokiuka haki za kimsingi za binadamu na sheria za kimataifa bila ya kujali nchi hizo zinachangia kiasi gani cha fedha katika bajeti yake na ujiepusha na siasa za kindumakuwili katika uwanja huo.