Iran: Israel haijali mstari wowote mwekundu wa maadili
(last modified Sun, 14 Jul 2024 07:06:52 GMT )
Jul 14, 2024 07:06 UTC
  • Iran: Israel haijali mstari wowote mwekundu wa maadili

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani vikali jinai mpya iliyofanywa na utawala wa Kizayuni katika eneo la Al-Mawasi huko Khan Yunis, kusini mwa Ukanda wa Gaza na kuua shahidi makumi ya wakimbizi wa Kipalestina na kujeruhi mamia ya wengine.

Nasser Kan'ani amesema katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa X kuwa: Kuvurumisha maroketi katika kambi za wakimbizi katika eneo la Al-Mawasi, magharibi mwa Khan Yunis, kusini mwa Ukanda wa Gaza, licha ya kutambuliwa kuwa maeneo salama, ni jinai nyingine katika msururu wa jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni.

Kan'ani ameeleza bayana kuwa, kwa kuendelea kumwaga damu za Wapalestina wasio na hatia katika maeneo mbali mbali ya Gaza, utawala wa Kizayuni umeidhihirishia dunia kuwa hautambui mstari wowote mwekundu wa maadili.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kimya cha jamii ya kimataifa mkabala wa mauaji dhidi ya wakimbizi wa Palestina wasio na ulinzi wala hatia huko Al-Mawasi, eneo ambalo utawala wa Kizayuni ulidai ni salama kwa ajili ya kukimbilia Wapalestina, kinakera na kusikitisha.

Nasser Kan'ani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran

Wizara ya Afya ya Ukanda wa Gaza imesema shambulio hilo la kinyama la jeshi la utawala wa Kizayuni katika eneo la Al-Mawasi huko Khan Yunis limepelekea kuuawa shahidi wakimbizi zaidi ya 90 wa Kipalestina wakiwemo wanawake na watoto wadogo, mbali na kujeruhiwa wengine zaidi ya 300.

Nasser Kan'ani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amebainisha kuwa, utawala katili wa Israel unaendelea kumwaga damu za Wapalestina kutokana na undumakuwili wa baadhi ya madola duniani, na ungaji mkono wa hali na mali wa Marekani na nchi za Ulaya. 

 

Tags