Iran: Kunyamazia kimya jinai za Wazayuni ni kuhamasisha jinai za wamwagaji damu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i114198-iran_kunyamazia_kimya_jinai_za_wazayuni_ni_kuhamasisha_jinai_za_wamwagaji_damu
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amegusia jinai zinazoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Ghaza na kulalamikia vikali kimya cha kuchupa mipaka cha jamii ya Kimataifa mbele ya jinai hizo za Wazayuni.
(last modified 2024-07-18T02:20:37+00:00 )
Jul 18, 2024 02:20 UTC
  • Iran: Kunyamazia kimya jinai za Wazayuni ni kuhamasisha jinai za wamwagaji damu

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amegusia jinai zinazoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Ghaza na kulalamikia vikali kimya cha kuchupa mipaka cha jamii ya Kimataifa mbele ya jinai hizo za Wazayuni.

Nasser Kan'ani Chafi,  ameandika katika mtandao wa kijamii wa X kwamba, utawala wa Kizayuni umefanya jinai nyingine ya kutisha katika skuli ya Al-Qahira mjini Ghaza kwa kuua kwa umati na kikatili, idadi kubwa ya raia wasio na hatia.

Katika shambulio hilo Wapalestina 11 wameuawa shahidi na wengine wengi kujeruhiwa kwa mkupuo mmoja.

Kan'ani Chafi ameongeza kuwa, kimya na kutochukua hatua serikali na mashirika ya kimataifa mbele ya ukatili, unyama na jinai zote hizi zinazofanywa na Wazayuni wafyonza damu za watu, kivitendo ni kuwaacha mikononi wazi makatili hao wafanye jinai na mauaji ya kimbari wanavyopenda huko Ghaza. 

Msemaji huyo wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran aidha amesisitiza kuwa, wale wanaodai kiuongo kuwa wanatetea haki za binadamu, ndio wafadhili wakuu wa silaha zinazotumiwa na Israel kufanya mauaji ya umati dhidi ya Wapalestina wasio na hatia. 

Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya ya Palestina katika Ukanda wa Ghaza, Wapalestina 38,794 wameshauawa shahidi na 89,364 wameshajeruhiwa kutokana na mashambulizi ya kikatili na kinyama kupindukia yanayoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni tangu tarehe 7 Oktoba 2023 huko Ghaza. Sehemu kubwa ya wahanga wa mashambulizi hayo ni wanawake na watoto wadogo.