Tehran inajiandaa kwa hafla ya kuapishwa Pezeshkian huku viongozi wa nchi mbalimbali wakiwasili kwa wingi
(last modified 2024-07-29T12:39:47+00:00 )
Jul 29, 2024 12:39 UTC
  • Masoud Pezeshkian
    Masoud Pezeshkian

Viongozi na maafisa wa ngazi ya juu kutoka nchi mbalimbali tayari wamewasili Tehran mji mkuu wa Iran kwa lengo la kushiriki katika hafla ya kuapishwa Rais mpya wa Iran, Masoud Pezeshkian kesho Jumanne.

Viongozi kutoka Cuba, Colombia, Mongolia, Malta, Niger, Libya, Gambia, Sudan, Mynmar, Ecuador, Jamhuri ya Dominican na Madagascar tayari wamewasili hapa Tehran. 

Viongozi wa nchi hizi na wengine kutoka nchi mbalimbali wanatazamiwa kushiriki katika hafla ya kuapishwa Rais mpya wa Iran Daktari Masoud Pezeshkian katika hafla itakayofanyika kwenye jengo la Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge), kesho mchana. 

Daktari Pezeshkian mwenye umri wa miaka 69 kesho ataapishwa rasmi kuwa Rais mpya wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mbele ya wawakilishi wa Bunge, Mkuu wa Idara ya Mahakama na wawakilishi wa Baraza la Kulinda Katiba. 

Hafla ya kuapishwa Rais mpya wa Iran itaonyeshwa moja kwa moja katika televisheni ya taifa na itaakisiwa na maripota, wapiga picha wa vyombo vya habari zaidi ya 600 vya ndani na nje ya nchi.

Tags