SEPAH: Malengo matukufu ya ukombozi wa Quds yamekaribia kufikiwa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i116904-sepah_malengo_matukufu_ya_ukombozi_wa_quds_yamekaribia_kufikiwa
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) ametoa ujumbe maalumu wa pongezi na wa mkono wa pole kufuatia kuuawa shahidi Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon na kusisitiza kuwa, malengo matukufu ya ukombozi wa Quds yamekaribia kufikiwa na historia itathibitisha hilo.
(last modified 2024-09-29T02:40:30+00:00 )
Sep 29, 2024 02:40 UTC
  • SEPAH: Malengo matukufu ya ukombozi wa Quds yamekaribia kufikiwa

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) ametoa ujumbe maalumu wa pongezi na wa mkono wa pole kufuatia kuuawa shahidi Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon na kusisitiza kuwa, malengo matukufu ya ukombozi wa Quds yamekaribia kufikiwa na historia itathibitisha hilo.

Kwa mujibu wa shirika la habari la FARS, Meja Jenerali Hassan Salami amesema hayo na kuongeza kuwa, jinai ya kinyama ya Wazayuni huko Beirut, mji mkuu wa Lebanon imefanyika kwa uungaji mkono wa wazi na wa kijuba wa Marekani bali kwa kushiriki pia viongozi wa Ulaya na Magharibi wanaodai kiuongo kuwa eti ni watetezi wa haki za binadamu ulimwenguni.

Katika ujumbe wake huo, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) amesema: Ni jambo lisilo na shaka kwamba Hizbullah ya Lebanon, HAMAS na kambi yote ya Muqawama itazidi kuwa imara na itaendeleza njia za kamanda huyu wa mashahidi kwa kutoa vipigo vikali zaidi hadi kuungamiza kabisa utawala pandikizi wa Kizayuni.

Sayyid wa Muqawama, shahid Hassan Nasrullah

Ijumaa usiku ndege za utawala wa Kizayuni zilifanya mashambulizi ya kikatili katika eneo la kusini mwa Beirut, mji mkuu wa Lebanon na kumuua shahidi Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon.

Sayyid Hassan Nasrullah ameuawa shahidi akiwa na umri wa miaka 64. Amefikia daraja takatifu ya kuuawa shahidi katika njia ya Allah baada ya kuwa Katibu Mkuu wa Hizbullah kwa muda wa miaka 32.