Umoja wa Umma wa Kiislamu, siri ya ushindi dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel
(last modified 2024-10-16T03:50:04+00:00 )
Oct 16, 2024 03:50 UTC
  • Umoja wa Umma wa Kiislamu, siri ya ushindi dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sambamba na kuleza kuwa Iran iko tayari kusaidia kujenga maelewano ya pamoja ya kiusalama kuhusu hatari ya kihistoria ya utawala wa Kizayuni, amesema: Kuna haja kusimamishwa aina yoyote ya mpango wa kisiasa na kiuchumi unaousaidia utawala huo ghasibu.

Mohammad Bagher Ghalibaf amesema hayo katika hotuba yake kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Mabunge (IPU) mjini Geneva Uswisi na kueleza jinsi utawala ghasibu wa Israel unavyotenda jinai za kinyama na mauaji ya kimbari dhidi ya ukanda wa Gaza na hivi sasa Lebanon.

Dakta Ghalibaf amesema, utawala ghasibu wa Israel umeacha hatua zote za kidhahiri na hivi sasa unafanya jinai dhidi ya Waislamu bila kujali chochote. Hili si jambo linalotokea Gaza au Lebanon pekee. Utawala dhalimu wa Israel una mpango mkubwa wa kurudia jinai hizo katika eneo lote la Kiislamu, na kwa uungaji mkono kamili wa Marekani na baadhi ya nchi za magharibi, unakusudia kufikia mahali ambapo ikilazimu ufanye chochote kile utakacho katika sehemu yoyote ile ya ulimwengu wa Kiislamu na jinai yoyote dhidi ya Kiongozi yeyote wa Kiislamu na uwe na kinga dhidi ya adhabu yoyote. Hili ni tatizo letu la pamoja.

Spika wa Bunge la Iran amehoji, hivi hatima imekuwa kwamba, ulimwengu wa Kiislamu uwe mtazamaji tu wa jinai za Israel?

Spika Ghalibaf sambamba na kubainisha kuwa, Israel inataka kudhibiti miundombinu yote ya eneo la Asia Magharibi ameongeza kuwa: Katika hali hii umoja na kusimama kidete ni sharti la usalama kwetu sisi sote.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake hiyo, Dakta Ghalibaf amesisitiza kuwa, Umma wa Kiislamu unapaswa kutoa mashinikizo jumuishi na madhubuti kwa Marekani ili kukomesha mauaji ya watoto yanayofanywa na Israel.

Muhammad Bagher Ghalibaf, Spika wa Bunge la Iran akizungumza na Dakta Tulia Ackson, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ndiye Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU).

 

Aidha amesema, mishipa muhimu ya uhai ya utawala wa Israel hivi sasa iko katika udhibiti wa Umma wa Kiislamu na bila shaka damu za mujahidina na wanamapambano na wanawake wanaodhulumiwa wa Lebanon na Palestina zitatoa baraka na Ulimwengu wa Kiislamu utaonja ladha ya siku tamu za kutokuweko Israel.

Viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima wamekuwa wakilitangaza suala la Palestina kuwa kipaumbele muhimu zaidi cha ulimwengu wa Kiislamu na kusisitiza ulazima wa umoja wa mataifa ya Kiislamu kwa thamani za pamoja za Kiislamu ili kutatua matatizo ya ulimwengu wa Kiislamu, hususan kuipatia ufumbuzi kadhia ya Palestina.

Kwa hakika umoja, mshikamano na ushirikishwaji wa Waislamu katika sehemu yoyote ya dunia hususan katika nchi za Asia Magharibi kuhusiana na masuala ya kistratijia ya Ulimwengu wa Kiislamu hususan katika kadhia ya Palestina na uvamizi wa Israel ni suala muhimu na la kimsingi. Kufanya mikutano ya kieneo na kimataifa kwa ajili ya kukaribiana mataifa ya Kiislamu, pamoja na kuundwa kwa miungano na taasisi za kimataifa, ni mojawapo ya mikakati ya kimsingi, lakini suala muhimu zaidi ni suluhisho la kivitendo na ushiriki wa pande zote kwa utekelezaji wa maamuzi na kutatua migogoro.

Licha ya kuweko misimamo yote ya nchi za Kiislamu dhidi ya uvamizi wa Israel, lakini matukio ya Palestina na Lebanon na kuendelea hujuma za Israel yanaonesha kuwa bila ya uungaji mkono wa kivitendo, dhulma wanayofanyiwa Waislamu haiwezi kuondolewa.

Kuhusiana na hilo, Spika wa Bunge la Iran amesema, kadiri mashinikizo ya wananchi dhidi ya serikali zenye uhusiano na utawala wa Kizayuni yanavyoongezeka, ndivyo suala hili linavyozidi kuwa na gharama kwao.

Zaidi ya Wapalestina 42,000 wameuawa shahidi tangu jeshi la Israel lilipoanza kufanya mashambulio dhidi ya Ukanda wa Gaza

 

Filihali, utawala wa Kizayuni unajaribu kuficha kushindwa kwake kushambulia vikosi vya muqawama na kupanua vita hadi Lebanon na vilevile kuendeleza uchokozi wake huko Gaza. Wazayuni pia wanataka kuzuia kuweko umoja wa Umma wa Kiislamu, na ili kufikia lengo hilo wanatumia mbinu chafu ya kuzusha hofu na mifarakano katika ulimwengu wa Kiislamu.

Ukweli ni kwamba, hivi sasa muqawama dhidi ya Uzayuni katika eneo umeelekeza matumaini yake kwa msaada wa Umma wa Kiislamu. Adui Mzayuni yuko katika hali tete zaidi katika historia yake na nchi za Kiislamu ziko katika nafasi ya kipekee ya kukomesha uovu huo wa kihistoria katika eneo. Kwa hiyo, umoja wa Umma wa Kiislamu na uungaji mkono wa kivitendo na madhubuti wa muqawama ndio njia pekee ya kumkwamisha adui Mzayuni.

Aidha katika mazungumzo yake pambizoni mwa mkutano wa Mabunge mjini Geneva, Spika wa Bunge la Iran alikutana na kufanya mazungumzo na maspika mbalimbali akiwemo Dakta Tulia Ackson, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ndiye Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU).

Tags