Ujenzi wa "nyumba zinazohamishika" huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel) kwa kuhofia makombora ya Hizbullah ya Lebanon
(last modified 2024-10-17T07:52:31+00:00 )
Oct 17, 2024 07:52 UTC
  • Ujenzi wa

Utawala wa Kizayuni wa Israel umeanza kutengeneza nyumba zinazohamishika kutokana na wasi wasi wa kuenea mashambulizi ya makombora ya Hizbullah ya Lebanon, ili kuendeleza shughuli za viwanda vya kaskazini mwa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na Israel.

Kwa mujibu wa ripoti ya kanali ya al Mayadeen siku ya Jumatano, Wizara ya Uchumi na Viwanda ya utawala wa Kizayuni imeweka makazi hayo katika maeneo kadhaa ya kaskazini kama vile "Shamir", "Yeroam", "Kefar Sald", "Rosh Pina" na "Delton"  kwa uafdhili wa wizara hiyo.

Zikiwa umbali wa kilomita 40 kutoka kwenye mpaka wa kaskazini wa Palestina inayokaliwa kwa mabavu, makazi hayo yanakusudiwa kutoa ulinzi wa haraka kwa wafanyakazi na wasimamizi wa viwanda vya maeneo hayo ambao wanakabiliwa na hali ngumu ya usalama kwenye mipaka ya kaskazini.

Utawala wa Kizayuni umeamua kuupanua mradi wa ujenzi wa nyumba za aina hiyo ambao kwa mara ya kwanza ulianza kutekelezwa huko Kiryat Shmona na hivi sasa umepanuliwa sana kutokana na ongezeko la mashambulizi ya Hizbullah dhidi ya viwanda vilivyoko katika miji ya kaskazini mwa ardhi hizo zinazokaliwa kwa mabavu.

Nir Barakat, Waziri wa Uchumi na Viwanda wa utawala wa Kizayuni amesema: "Ulinzi wa viwanda si suala la usalama tu, bali ni hitajio la kiuchumi na tunahitaji kuendeleza uzalishaji katika maeneo ya kaskazini."

Tangu tarehe 23 Septemba, jeshi la Kizayuni limefanya mashambulizi makubwa katika maeneo mbalimbali ya kusini mwa Lebanon ambapo Hizbullah ya Lebanon imeanzisha  oparesheni kadhaa dhidi ya vituo vya kijeshi  na vitongoji vya walowezi wa Kizayuni kaskazini mwa Palestina katika kulipiza kisasi cha utawala huo katili kushambulia raia wa Lebanon.

Kufuatia kupanuka kwa mashambulizi ya makombora ya Hizbullah katika miji ya Safed na Haifa, utawala huu unakabiliwa na kupungua kwa shughuli za kiviwanda na kibiashara kutokana na kupungua kwa idadi ya wafanyakazi na kufungwa kwa viwanda vya kaskazini mwa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na Israel.

Tags