Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran aanza safari barani Afrika
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran leo ameondoka hapa mjini Tehran na kuanza safari ya kuzitembelea nchi kadhaa za magharibi mwa Afrika.
Akiuongoza ujumbe wa ngazi za juu wa kisiasa na kiuchumi wa Iran, Dakta Muhammad Javad Zarif leo ameondoka Tehran na kuelekea Abuja, Nigeria ikiwa ni kituo chake cha kwanza katika safari yake ya kuzitembelea nchi kadhaa za Afrika Magharibi.
Mbali na Nigeria, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran atazitembelea pia nchi za Ghana, Guinea-Conakry na Mali.
Lengo la safari hiyo ni kufanya juhudi za kuimarisha zaidi ushirikiano kati ya Iran na nchi za magharibi mwa Afrika.
Katika safari yake hiyo ya situ sita, Dakta Javad Zarif atakutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa ngazi za juu wa nchi hizo sambamba na kushiriki katika mikutano ya wadau wa masuala ya kibiashara.
Hii ni duru ya tatu ya safari ya Dakta Javad Zarif barani Afrika ambapo Agosti mwaka jana alifanya safari katika eneo la kaskazini mwa Afrika. Akiwa huko alizitembelea nchi za Tunisia na Algeria.
Aidha Februari mwaka jana, Waziri wa Mashauri ya Kigeni ya Iran alifanya safari Afrika Mashariki na kuzitembelea nchi za Kenya, Uganda, Burundi na Tanzania na kufanya mazungumzo na viongozi mbalimbali wa nchi hizo.