Ghalibaf: Changamoto ya uhusiano wa kiuchumi wa Iran na Afrika ni usafiri
(last modified Fri, 17 Jan 2025 07:21:44 GMT )
Jan 17, 2025 07:21 UTC
  • Ghalibaf: Changamoto ya uhusiano wa kiuchumi wa Iran na Afrika ni usafiri

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) ameyataja matatizo ya usafiri kuwa ni miongoni mwa changamoto kubwa katika kupanua uhusiano wa kiuchumi wa Iran na bara la Afrika akisema: Uwezo wa kimataifa kama wa kundi la BRICS na Shanghai ni fursa muhimu za kustawisha ushirikiano wa kiuchumi.

Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Bagher Ghalibaf, ambaye yuko safarini kikazi nchini Ethiopia amekutana na kufanya mazungumzo na kundi la wanaharakati wa masuala ya kiuchumi wa Iran wanaoishi Ethiopia baada ya kuwasili Addis Ababa Alkhamisi jioni.

Katika kikao hicho Ghalibaf amesisitizia ulazima wa kutumiwa uwezo wa kimataifa kama vile BRICS na Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai na kusisitiza kwamba: Licha ya vikwazo, uwepo wa Iran katika mashirika hayo umetoa fursa muhimu kwa maendeleo ya ushirikiano wa kiuchumi.

Spika wa Bunge la Iran ametaja matatizo ya usafiri kuwa moja ya changamoto kubwa katika kupanua uhusiano wa kiuchumi wa Iran na nchi za Afrika na kusema: "Ukosefu wa miundombinu endelevu ya usafiri umefanya mchakato wa biashara na bara hilo kuwa mgumu. Zaidi ya hayo, ushiriki wa sekta binafsi katika eneo hili ni mdogo na hasa taasisi zisizo za kiserikali."

Spika wa Bunge la Iran amesisitizia ulazima wa kushirikiana na nchi nyingine ili kuondoa baadhi ya vikwazo na kusema: “Kwa ushirikiano wa baadhi ya nchi kama vile China, tunaweza kupunguza matatizo yanayohusiana na SWIFT na uhamishaji fedha. 

Katika mkutano huo wanaharakati wa masuala ya kiuchumi wa Iran walioko nchini Ethiopia wameelezea matatizo yao katika uwekezaji na biashara nchini humo na kubainisha kuwa miongoni mwa matatizo hayo ni mabadiliko ya mara kwa mara ya sera za sarafu na kodi na gharama kubwa za usafirishaji kutokana na kukosekana miundombinu imara katika njia mbalimbali za bara la Afrika.