Araghchi: Netanyahu 'anaiamuru waziwazi' Marekani cha kufanya katika mazungumzo na Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i128302
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, waziri mkuu wa utawala wa kizayuni wa Israel ameshindwa kufikia lolote kati ya malengo ya vita vya karibuni vya utawala huo ghasibu dhidi ya Iran.
(last modified 2025-07-15T05:05:40+00:00 )
Jul 14, 2025 03:30 UTC
  • Araghchi: Netanyahu 'anaiamuru waziwazi' Marekani cha kufanya katika mazungumzo na Iran

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, waziri mkuu wa utawala wa kizayuni wa Israel ameshindwa kufikia lolote kati ya malengo ya vita vya karibuni vya utawala huo ghasibu dhidi ya Iran.

Sayyid Abbas Araghchi amebainisha kuwa Benjamin Netanyahu "anaamuru waziwazi" kile ambacho Marekani inapaswa kusema au kufanya katika majadiliano na Iran, licha ya kushindwa katika uchokozi wa hivi karibuni dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Araghchi ameyasema hayo katika andiko aliloweka kwenye mtandao wa kijamii akijibu matamshi ya Netanyahu aliyedai kwamba Iran lazima ipunguze masafa yanakofika makombora yake hadi kilomita 480.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amebainisha kuwa ni dhihaka na upuuzi kutarajia Iran ikubali ushauri kutoka kwa "mhalifu wa vita."

Amesisitiza kuwa, matarajio ya Netanyahu ya kudhoofisha zaidi ya miaka 40 ya maendeleo ya amani ya nyuklia hayaendani na uhalisia.

Araghchi amebainisha kwamba kila mmoja kati ya wanasayansi kadhaa wa Iran waliouliwa shahidi na mamluki wa Wazayuni walishatoa mafunzo kwa warithi wao100 wenye uwezo, ambao watamuonyesha Netanyahu uwezo wao.

"Lakini kiburi chake hakiishii hapo. Kwa kushindwa vibaya kufikia hata moja katika malengo yake ya vita nchini Iran na kulazimika kumgeukia 'Baba' wakati makombora yetu yenye nguvu yalipolenga maeneo ya siri ya Israel- ambayo Netanyahu angali anachuja taarifa zake- sasa anaamuru kwa uwazi nini Marekani inapaswa iseme au isiseme katika mazungumzo na Iran," ameongezea kusema Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran.

Mnamo Juni 13, utawala wa kizayuni ulianzisha uchokozi wa wazi na usio na msingi dhidi ya Iran, na kuwaua makamanda wengi wa ngazi za juu wa kijeshi, wanasayansi wa nyuklia, na raia wa kawaida.

Zaidi ya wiki moja baadaye, Marekani pia iliingia vitani kwa kushambulia vituo vitatu vya nyuklia vya Iran katika ukiukaji mkubwa wa Hati ya Umoja wa Mataifa, sheria za kimataifa na mkataba wa NPT.

Katika kujibu jinai hizo, Iran ilitekeleza Operesheni ya Ahadi ya Kweli III, ya mashambulio makali yaliyotwanga na kuteketeza miundombinu muhimu ya kijeshi, ya kijasusi na ya kiviwanda ya utawala wa kizayuni.

Operesheni hiyo ilihusisha mamia ya makombora ya balestiki na ndege zisizo na rubani zilizovuruga mitambo ya Israel ya kutungua makombora na kusababisha uharibifu mkubwa kote Tel Aviv, Haifa na Be'er Sheva.

Mbali na mashambulizi hayo ya kulipiza kisasi dhidi ya utawala wa Kizayuni vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vilitekeleza pia operesheni ya shambulio la makombora dhidi ya kituo kikuu cha jeshi la anga cha Marekani cha Al-Udeid kilichoko nchini Qatar.

Kutokana kushadidi mashambulio ya makombora ya Iran yaliyojumuisha makombora ya kisasa zaidi, mnamo Juni 24, utawala bandia wa Israel ulilazimika kutangaza kusimamisha uvamizi wake kwa upande mmoja, ambao ulitangazwa kwa niaba yake na rais wa Marekani.../

.