Safari ya Zarif Uturuki; fupi lakini ya mafanikio mengi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Muhammad Javad Zarif, siku ya Ijumaa alifanya safari ya siku moja nchini Uturuki; safari fupi lakini iliyokuwa na mafanikio mengi. Katika safari yake hiyo Zarif alikutana na kufanya mazungumzo na waziri mwenzake wa Uturuki pamoja na Rais wa nchi hiyo.
Alipowasili uwanja wa ndege wa Ankara siku hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alifanya mazungumzo mafupi na waandishi wa habari ambapo aliashiria matukio ya karibuni hususan jaribio la mapinduzi ya kijeshi ya Julai 15 nchini Uturuki.Kwa kulaani jaribio hilo lililoshindwa Dakta Zarif alionyesha kuwa mtazamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa usalama wa majirani zake si mtazamo wa kijuujuu na wa sehemu fulani tu. Alisema: "Iran ililaani hatua ya wafanya mapinduzi katika saa ileile ya jaribio lile kwa sababu sisi tunaamini kuwa mapinduzi ya kijeshi hayana nafasi katika eneo; na kura za wananchi na matakwa ya wananchi hayawezi kukandamizwa na hatua ya kundi fulani la kijeshi".
Matamshi hayo yameonyesha kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alielekea mjini Ankara na muelekeo wa kuzingatia maslahi na usalama wa pamoja; na ni kwa msingi huo ndio maana alipokutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Mevlüt Çavuşoğlu na Rais wa nchi hiyo Recep Tayyip Erdoğan walijadili masuala ya pande mbili, ya kieneo na kimataifa.
Uhusiano wa Iran na Uturuki katika miaka ya karibuni, ambapo eneo hili limekuwa kwenye mtikisiko wa tufani na dhoruba za vita na machafuko, umeshuhudia mchanganyiko wa shwari na hamkani; hata hivyo pande mbili za Tehran na Ankara zimeweza kwa namna fulani kuwa na uratibu mzuri wa hitilafu zao za mitazamo. Na ni sababu hiyo ndiyo iliyoifanya mitazamo ya nchi mbili hizi iwe ya kuzingatia zaidi matatizo na changamoto za pamoja badala ya kujali zaidi fursa na maslahi ya muda. Ni kama alivyoeleza Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki aliposifu na kupongeza misimamo ya Iran ya kuunga mkono serikali ya nchi hiyo kwa kusema:"Wakati kulipokuwa hakuna muelekeo wowote wa wazi juu ya hali ya mambo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alieleza mara kadhaa kupitia mazungumzo ya simu uungaji mkono wake kwa serikali na wananchi wa Uturuki dhidi ya wafanyamapinduzi".
Kwa maelezo haya, wachambuzi na wafuatiliaji wengi wa masuala ya Mashariki ya Kati wanaitathmini safari ya Zarif mjini Ankara katika mazingira yaliyopo kuwa ni muendelezo wa kikao cha hivi karibuni cha pande tatu za Iran, Uturuki na Russia. Kwa mtazamo wa wachambuzi hao nchi hizi tatu ni wadau muhimu katika eneo na kuna haja ya kuzungumza na kuwepo ushirikiano baina yao. Na kwa hivyo, hata kama zitakuwepo hitilafu za mitazamo inapasa zitatuliwe kupitia mazungumzo.
Kwa kuyatupia jicho la haraka haraka matukio ya eneo inatupasa tuseme kuwa hali ya mvurugiko na mchafukoge ya Mashariki ya Kati imegubika kila kitu. Macho yote yameelekezwa kwenye matukio ya Syria na Iraq na kukabiliana kwa hali zote na makundi ya kigaidi, huku mazungumzo ya kila mahala yakiwa ni juu ya namna ya kushirikiana katika mapambano hayo.
Kuhusiana na nukta hii, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki amesema kuimarishwa ushirikiano wa Iran na Uturuki ni kwa madhumuni ya kuleta suluhu na amani ya kudumu nchini Syria na kuongeza kwamba Tehran na Ankara zina fikra moja kuhusu kulindwa umoja wa ardhi yote ya Syria; na kwamba kuendelea mazungumzo baina ya nchi mbili kuna nafasi chanya katika kutekelezwa ustishaji vita wa kudumu nchini humo.
Wakati huohuo, baada ya mazungumzo kwa njia ya simu yaliyofanywa wiki iliyopita kati ya Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki vyombo vya habari vya Russia vimezungumzia uwezekano wa kushirikiana nchi hiyo, Iran na Uturuki kwa ajili ya kuutatua mgogoro wa Syria. Siku ya Alkhamisi iliyopita ubalozi wa Russia hapa nchini ulitangaza kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo Mikhail Bogdanov kesho Jumatatu anatazamiwa kufanya safari hapa nchini Iran kwa madhumuni ya kujadili matukio na masuala ya eneo hususan mgogoro wa Syria.
Suala la Syria hivi sasa ndicho kipaumbele cha jitihada mbalimbali zinazofanywa kieneo. Mnamo siku chache zijazo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry na Makamu wa Rais wa nchi hiyo Joe Biden watafanya safari kuelekea nchini Uturuki. Katika mazingira kama haya haifai hata kidogo kuipoteza fursa ya mazungumzo. Iran imekuwa kila mara ikisisitiza kuhusu kurejeshwa uthabiti nchini Syria; imani na msimamo ambao ndio ilionao hadi sasa. Ila kitu pekee kilichobadilika wakati huu ni kwamba hivi sasa pande zote, ikiwemo hata Marekani, zimeshatambua kuwa ugaidi ni kitisho kinachozikabili nchi zote. Na kwa sababu hiyo kuna ulazima wa kupambana na magaidi wote wakiwemo wa Daesh na Jabhatu-Nusra. Hivi sasa Uturuki nayo inakubaliana na udharura wa kuzidishwa ushirikiano juu ya suala hilo.
Tab'an kutokana na tajiriba ya matukio yaliyojiri huko nyuma, kubadilika misimamo ya Uturuki ni jambo lililokuwa likitarajiwa. Ni wazi kwamba hivi sasa tutashuhudia mageuzi ya msingi katika kadhia ya Syria na Mashariki ya Kati (Magharibi mwa Asia). Bila ya shaka kungali kuna mafundo ambayo bado hayajaweza kufunguliwa; hivyo tusubiri kuona hatua haribifu za Wasaudia na jibu na radiamali zao kwa mabadiliko yanayojiri hivi sasa katika eneo itakuwaje.../