Waziri Araghchi aanika nafasi ya Marekani, Israel katika ghasia za Iran
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araghchi amezionya vikali Marekani na utawala haramu wa Israel juu ya matokeo mabaya ya uchochezi na uungaji mkono wao kwa wafanya fujo na wazua rabsha hapa nchini, akisisitiza kuwa Washington na Tel Aviv zinataka kuyageuza maandamano ya kiuchumi ya wananchi wa Iran kuwa machafuko na ghasia.
Araghchi ameyasema hayo katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa X jana Jumamosi, ambapo amemnukuu mkurugenzi wa zamani wa shirika la ujasusi la Marekani CIA, Mike Pompeo akithibitisha nafasi na mchango wa shirika la kijasusi la Israel Mossad katika ghasia hizo.
Kwa mujibu wa Mwanadiplomasia huyo mkuu, hatua ya Pompeo kukiri katika ujumbe wa X mapema mwezi huu, kunapingana na madai ya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu, akisisitiza kuwa ghasia zinazoshuhudiwa nchini zimechochewa na maafisa wa Tel Aviv na Washington.
"Mkurugenzi wa zamani wa CIA wa Rais Trump mwenyewe ameangazia waziwazi na bila aibu kile Mossad na wawezeshaji wake wa Marekani wanafanya," Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameeleza na kuongeza kuwa, Marekani na waitifaki wanaamini kwa njozi kuwa, "hatimaye uchomaji hauwachomi [wachomaji]."
Aidha jana Jumamosi, Rais Masoud Pezeshkian alisema Marekani imekosea kwa kuamini kwamba, mbinu zake dhidi ya maadui wengine katika nchi nyingine, zinaweza kutumika dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu, akisisitiza kwamba wananchi wa Iran wanaendelea kuwa macho mkabala wa juhudi zozote za kuiyumbisha nchi.
Wakati huo huo, Shirika la Intelijensia la Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limetangaza habari ya kumtia mbaroni raia wa kigeni anayehusika na ujasusi kwa niaba ya shirika la kijasusi wa utawala wa Israel Mossad.
Shirika hilo liliripoti habari hiyo katika taarifa ya jana Jumamosi, likisema kuzuiliwa huko kumekuja huku kukiwa na juhudi kubwa za kukabiliana na majaribio yanayoungwa mkono na mataifa ya kigeni ya kuyumbisha nchi. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mtu huyo aliingia Iran kwa siri, kuja kukusanya taarifa za kijasusi kwa niaba ya Mossad na kutathmini operesheni za kigaidi za maajenti wa shirika hilo.