Kwa nini Pakistan imekosoa msimamo wa Trump kuhusu machafuko nchini Iran?
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i135474-kwa_nini_pakistan_imekosoa_msimamo_wa_trump_kuhusu_machafuko_nchini_iran
Pakistan imekosoa msimamo wa Rais Donald Trump wa Marekani kuhusu machafuko yanayochochewa na nchi za Magharibi nchini Iran.
(last modified 2026-01-14T07:21:32+00:00 )
Jan 14, 2026 07:21 UTC
  • Kwa nini Pakistan imekosoa msimamo wa Trump kuhusu machafuko nchini Iran?

Pakistan imekosoa msimamo wa Rais Donald Trump wa Marekani kuhusu machafuko yanayochochewa na nchi za Magharibi nchini Iran.

Khawaja Muhammad Asif, Waziri wa Ulinzi wa Pakistan, ambaye amekuwa akikosoa ushirikiano wa Marekani na utawala wa Kizayuni katika mauaji ya halaiki ya Wapalestina, huku akigusia uingiliaji wa Marekani katika masuala ya ndani ya Iran, amemtaka Rais Trump wa nchi hiyo asimamishe kikweli mauaji ya Gaza ili kuzuia kuendelea jinai za Israel katika ukanda huo.

Khawaja Muhammad Asif ambaye ni mpinzani mkubwa wa siasa za uchochezi za Marekani katika eneo ameguswa na mitazamo miwili inayogongana ya Rais Donald Trump wa Marekani kuhusu Iran na uuungaji mkono wake kwa utawala wa Kizayuni wa Israel. Akiwa na kumbukumbu kamili ya unafiki wa Trump kuhusu amani na eti kusaidia kukomesha vita, ameandika kwenye akaunti yake rasmi ya mtandao wa kijamii wa X kwamba rais wa Marekani ana uwezo wa kuingilia kati na kukomesha mauaji ya Wapalestina huko Gaza.

Waziri wa Ulinzi wa Pakistan ameongeza kuwa: "Ulimwengu mzima umeungana dhidi ya mauaji ya halaiki ya Wapalestina na uvamizi wa Israel, lakini badala ya kuingilia kati na kukomesha jinai hizo, Marekani inaendelea kuipa silaha Israel na hivyo kuchangia mauaji ya Gaza."

Wiki iliyopita, Waziri wa Ulinzi wa Pakistani aliutaja utawala wa Kizayuni kuwa mtendajinai anayechukiwa zaidi katika historia na kuongeza: 'Huenda Marekani ilidanganywa na uwongo wa Netanyahu, au wote wawili hao wanashirikiana katika vitendo vya chuki dhidi ya Iran.' Amesisitiza kuwa, Waziri Mkuu wa Utawala wa Kizayuni daima amekuwa akisema uwongo dhidi ya miradi ya nyuklia ya amani ya Iran, lengo lake likiwa ni kuhalalisha uchokozi dhidi ya Iran katika siku zijazo.

Pia wataalamu wengi, raia na maafisa wa Pakistan wanaofuatilia matukio ya hivi karibuni nchini Iran wanasema: 'Tehran kamwe haitasalimu amri mbele ya matakwa haramu na ya kibeberu ya Ulaya na Marekani, na mara hii pia itasambaratisha njama za Magharibi na Israel dhidi yake.' Miongoni mwao ni, Sirajul Haq, mkuu wa zamani wa Jamaat-e-Islami ya Pakistan, ambaye amekosoa undumakuwili wa Trump kuhusu mauaji ya Wapalestina na uungaji mkono wake kwa magenge yanayovuruga usalama wa Iran na kuandika: 'Wakati Donald Trump akiendeleza uungaji mkono wake mkubwa wa kisiasa na kijeshi kwa Tel Aviv kwa kumkaribisha rasmi huko White House muhusika mkuu wa mauaji ya Wapalestina na mchinjaji wa Gaza, Netanyahu, sambamba na kukuza kupita kiasi mkusanyiko wa waandamanaji kadhaa nchini Iran, anajaribu kujionyesha kuwa mtetezi wa haki za binadamu. Mbinu hii kwa hakika ni kejeli kubwa kwa viwango na maadili ya kimataifa.'

Umati mkubwa wa wananchi wakiunga mkono serikali dhidi ya uchochezi wa nchi za Magharibi

Inaonekana ukosoaji wa Pakistan dhidi ya msimamo wa Donald Trump kuhusu machafuko ya Iran umejikita katika masuala ya kijiografia, kisiasa, kiusalama na kidiplomasia. Msimamo wa Trump unajumuisha vitisho vya "kuingilia kati" na maonyo makali dhidi ya Tehran, ambayo kwa kawaida yameamsha hisia za nchi jirani za Iran, ikiwa ni pamoja na Pakistan.

Sababu ya kwanza ya ukosoaji wa Pakistan ni wasiwasi wa kukosekana utulivu wa eneo. Kuongezeka mvutano kati ya Iran na Marekani kunaweza kuwa na taathira za moja kwa moja za usalama kwa Pakistan. Uzoefu wa miaka iliyopita unaonyesha kuwa hata uwezekano wa kutokea mashambulizi au mashinikizo ya kijeshi ya Marekani dhidi ya Iran unaiweka Islamabad katika hali ngumu, kama ilivyofanyika mwaka 2025, ambapo Pakistan ilionya dhidi ya mashambulizi ya Marekani dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran na kulitaja suala hilo kuwa ukiukaji wa sheria za kimataifa.

Sababu ya pili ni wasiwasi kuhusu matokeo ya kibinadamu na kiuchumi. Katika miaka ya hivi karibuni, Pakistan imekariri kwamba mgogoro wowote nchini Iran unaweza kuvuruga biashara ya mpakani na hivyo kuibua mashinikizo ya kiuchumi katika eneo. Hii inaonesha kuwa, Islamabad inachukulia machafuko nchini Iran kuwa tishio la moja kwa moja kwa usalama wake na ina wasiwasi kuhusu kuchochewa machafuko hayo na Marekani na utawala wa Kizayuni.

Sababu ya tatu ni sera za kigeni za Pakistan. Islamabad daima imekuwa ikisisitiza udharura wa nchi za kigeni kutoingilia masuala ya ndani ya nchi za eneo. Ukosoaji wa Islamabad dhidi ya msimamo wa Trump kuhusu Iran pia unaweza kutathminiwa katika fremu hiyo hiyo hususan katika hali ambayo uhusiano wake na Tehran una umuhimu mkubwa kwa usalama wa mipaka ya pamoja. Aidha Pakistan imekuwa ikikosoa mara kwa mara msimamo wa Marekani katika kuunga mkono utawala wa Kizayuni katika mauaji yake ya kimbari dhidi ya Wapalestina huko Gaza.

Sababu ya nne inahusiana na mambo ya ndani. Wananchi wa Pakistan na wanasiasa wengi wa nchi hii wametangaza mara nyingi uungaji mkono wao kwa Iran mbele ya sera na hatua za kichokozi na zisizo halali za Marekani dhidi ya taifa hili. Wakati huo huo, uzoefu wa majibu makali ya Iran dhidi ya matamshi ya uingiliaji kati ya Trump na maafisa wa serikali yake unaonyesha kuwa Tehran inachukulia uungaji mkono wowote kwa mashinikizo ya kigeni kuwa ni uingiliaji wa masuala yake ya ndani.

Kwa ujumla, ukosoaji wa Pakistan kuhusu msimamo wa hivi karibuni wa Trump unatokana na mchanganyiko wa masuala ya usalama, uchumi, sera za kigeni na haja ya kudumishwa uwiano wa kikanda, mambo yaliyoipelekea Islamabad kuchukua msimamo mkali dhidi ya matamshi ya kichokozi ya Washington.