Rezaei: Tutazishughulikia balozi za Ujerumani, Uingereza na Ufaransa kwa kufanya uhalifu Iran
Msemaji wa Kamati ya Usalama wa Taifa na Sera za Kigeni ya Bunge la Iran amesema: Mabalozi wa nchi kama vile Ujerumani, Uingereza na Ufaransa ndio waliochochea ghasia na kusimamia vitendo vya kigaidi vya hivi karibuni nchini Iran na kwamba Tehran itazishughulikia balozi hizo.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Fars, Ebrahim Rezaei, amesema hayo katika mazungumzo na waandishi wa habari usiku wa kuamkia leo Jumapili akiwa Bushehr, kusini mwa Iran na kusema: "Tuna taarifa kwamba nchi za Magharibi zimewapa msaada wa kifedha magaidi na kugawa dola za kuchochea ghasia na mauaji ndani ya Iran, na nchi hizo lazima tutazishughulikia, kwa sababu zimefanya jinai na uhalifu ndani ya Iran."
Amesema: "Kupanga vigenge vipya vya kigaidi katika miji mbalimbali ya Iran ili kuchochea mauaji kupitia kutoa mwito wa kujitokeza "katika siku iliyoahidiwa" na kuahidi malipo ya fedha za kigeni kwa magaidi hao, ni sehemu ya uchochezi wa mauaji na ghasia uliofanywa na balozi za nchi hizo za Magharibi.
Akizungumzia matukio ya Januari 8 na 9, msemaji wa Kamati ya Usalama wa Taifa na Sera za Kigeni ya Majlisi ya Ushauri wa Kiislamu yaani Bunge la Iran amesema: Ghasia na mauaji ya watu katika siku hizo yalipangwa na kuungwa mkono na Marekani na utawala wa Kizayuni; yalikuwa ni muendelezo wa vita vilevile vya vya siku 12, na kwamba siku hizo za Januari 8 na 9, 2026 zilikuwa ni siku za 13 na 14 za vita vya siku 12.
Vilevile amesema: Vikosi vya usalama vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vimekamata kiasi kikubwa cha silaha na kuwatia mbaroni mamluki wengi wa kigeni na vyote hivyo ni sehemu ya ushahidi wa kuhusika moja kwa moja balozi hizo za Ujerumani, Uingereza na Ufaransa katika mauaji na ghasia za hivi karibuni nchini Iran.