Washauri wa kijeshi wa Iran wako Syria kwa ombi la nchi hiyo
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i1408-washauri_wa_kijeshi_wa_iran_wako_syria_kwa_ombi_la_nchi_hiyo
Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran Mohammad Javad Zarif anasema washauri wa kijeshi wa Iran wako Syria kufuatia ombi la serikali ya nchi hiyo ya Kiarabu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 17, 2016 03:50 UTC
  • Washauri wa kijeshi wa Iran wako Syria kwa ombi la nchi hiyo

Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran Mohammad Javad Zarif anasema washauri wa kijeshi wa Iran wako Syria kufuatia ombi la serikali ya nchi hiyo ya Kiarabu.

Akihutubu katika Bunge la Umoja wa Ulaya mjini Brussels Jumanne, Zarif amepuuzilia mbali madai katika baadhi ya vyombo vya habari kuwa Iran imetuma wanajeshi wake kupigana kwa niaba ya serikali ya Rais Bashar al Assad. Amesema Iran haina askari wa nchi kavu Syria na kwamba walioko nchini humo kutoka Iran ni washauri wa kijeshi tu ambao wametumwa nchini humo kufuatia ombi la serikali ya Syria.

Ameongeza kuwa: "Kumekuwepo washarui wa kijeshi kufuatia ombo la Syria. Tutaondoa washauri hao wa kijeshi wakati serikali ya nchi hiyo itakapoona hali inaruhusu."

Zarif amesema serikali ya Syria ni halali na inatambuliwa na Umoja wa Mataifa na kwa hivyo wale ambao wanachukua hatua dhidi ya nchi hiyo bila idhini wanakiuka kanuni za kimataifa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuhusu umuhimu wa kumalizwa mapigano Syria na kusema ni taifa la Syria ndilo lililo na uwezo wa kuamua hatima ya nchi hiyo.

Magaidi wanaopata himaya ya kigeni walianzisha mapigano Syria mwaka 2011 na hasi sasa watu karibu nusu milioni wameuawa na wengine milioni sita kuwa wakimbizi ndani ya nchi huku milioni nne wakikimbilia nchi za kigeni.