Larijani: Marekani inachochea ugaidi kupitia vita
Spika wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu yaani Bunge la Iran amesema Marekani inachochea ugaidi katika eneo hili la Mashariki ya Kati na duniani kote kwa ujumla kwa kutumia anga ya vita na mapigano.
Ali Larijani, Spika wa Bunge la Iran ameyasema hayo katika mazungumzo na Přemysl Sobotka, Naibu Mwenyekiti wa Bunge la Seneti la Jamhuri ya Czech hapa mjini Tehran na kuongeza kuwa, makundi ya kigaidi yanayoungwa mkono na Marekani yanahatarisha usalama na uthabiti sio tu katika eneo hili bali kote duniani.
Larijani ameongeza kuwa, juhudi za kikweli na irada ya kisiasa inahitajika ili kuung'oa ugaidi na mizi yake na kusisitiza kwamba, ili kufanikiwa katika hilo, kampeni ya pamoja ya kimataifa inahitajika.
Kuhusu duru mpya ya mazungumzo ya kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa Syria huko mjini Lausanne nchini Usiwsi, Spika wa Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu amesema kuwa, mazungumzo hayo yamegonga mwamba kama ilivyotarajiwa huku akisisitizia umuhimu wa kushughulikia zaidi mizizi ya ugaidi badala ya athari zake.
Kwa upande wake, Naibu Mwenyekiti wa Seneti ya Jamhuri ya Czech amesema makundi ya kigaidi yamechipuka na kupata nguvu kutokana na tabia ya nchi za kibeberu kuingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine. Amesema kuwa Prague iko tayari kuimarisha ushirikiano wake na Tehran katika vita dhidi ya ugaidi duniani.