Wairani waungana na dunia katika kumbukumbu ya Arubaini ya Imam Hussein AS
Wananchi wa matabaka yote wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wameungana na dunia katika kumbukumbu ya Arubaini ya Imam Hussein AS, mjukuu wa Mtume Muhammad SAW, aliyeuawa shahidi katika jangwa la Karbala nchini Iraq, mwaka wa 61 Hijria.
Mamia ya maelfu ya Wairani wa matabaka yote, vijana kwa wazee, wake kwa waume wameungana katika marasimu mbalimbali ya kukumbuka siku hii tokeo jana.
Baadhi wameshiriki katika shughuli za Arubaini ya Imam Hussein AS kwa maandamano huku wengine wakikusanyika katika vituo mbalimbali vya kidini katika pembe zote za nchi. Hapa mjini Tehran sawa na maeneo mengi ya nchi, wananchi Waislamu wa Iran wamefanya matembezi ya Arubaini licha ya mvua, theluji na baridi kali.
Mbali na kushiriki marasimu mbalimbali humu nchini, idadi kubwa ya Wairani pia imesafiri hadi Karbala nchini Iraq kushiriki katika kumbukumbu ya Arubaini ya Imam Hussein (as).
Siku ya Ijumaa Waziri wa Usalama wa Ndani wa Iran alisema mamilioni ya watu wamejitokeza kwa wingi na kwa hamasa kubwa kushiriki katika matembezi ya Arubaini ya Imam Hussein AS mwaka huu na kuongeza kuwa, kujitokeza kwa wingi kiasi chote hicho kumeufanya uwezo wa mpaka wa ardhini wa Iran na Iraq huko Mahran ufikie kikomo na usiwe na uwezo tena wa kupokea watu zaidi.
Inafaa kukumbusha hapa kuwa, matembezi, majlisi na ziara ya siku ya Arubaini hufanyika kila mwaka tarehe 20 Safar, kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Qamaria, baada ya kupita siku arubaini tangu tarehe 10 mwezi wa Muharram kwa ajili ya kukumbuka kuuawa shahidi mjukuu wa Mtume SAW, Imam Hussein AS na masahaba zake ambao walijitolea roho zao kwa ajili ya kuhuisha dini ya Mwenyezi Mungu katika jangwa la Karbala.
Maafisa wa serikali ya Iraq wanatabiri kuwa watu zaidi ya milioni 20 watashiriki katika matembezi ya Arubaini ya Imam Hussein AS mwaka huu. Iraq inatazamiwa kuadhimisha siku hii tukufu kesho Jumatatu.