Nov 26, 2016 15:59 UTC
  • Iran yaomboleza kifo cha Fidel Castro

Rais Hassan Rouhani wa Iran ametuma salamu za rambirambi kwa taifa na serikali ya Cuba kufuatia kuaga dunia Fidel Castro, Kiongozi wa Mapinduzi ya nchi hiyo ya Amerika ya Latini.

Katika ujumbe wake huo Rais Rouhani amesema amepokea kwa masikitiko makubwa habari ya kifo cha Kiongozi wa Mapinduzi ya Cuba ambaye amemtaja kuwa mwanamapambano ambaye hakuchoka.

Rais Rouhani amesema, katika zama hizi ambapo mataifa yaliyodhulumiwa duniani yamenyimwa haki za kimsingi za ubinadamu kama vile amani, uadilifu na uhuru, kwa bahati nzuri kumekuwepo viongozi kama Fidel Castro ambaye aliendeleza mapambano hadi lahadha za mwisho za maisha yake. Amesema Fidel alibeba bendera ya kutetea uhuru wa walimwengu.

Rais Rouhani akiwa na hayati Fidel Castro Sept. 19 2016 mjini Havana

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran Mohammad Javad Zarif amesema hayati Fidel Castro, Kiongozi wa Mapinduzi ya Cuba alikuwa kigezo katika mapambano ya uhuru ya mataifa yaliyodhulumiwa.

Katika ujumbe wake Jumamosi ya leo kwa taifa na serikali ya Cuba baada ya kutangazwa kifo cha Fidel Castro, Zarif ameongeza kuwa, kiongozi huyo alikuwa shakhsia wa kipekee katika mapambano dhidi ya ukoloni na ubeberu.

Mapema leo Serikali ya Cuba ilitangaza habari ya kufariki dunia Fidel Alejandro Castro Ruz, rais wa zamani wa nchi hiyo akiwa na umri wa miaka 90.

Tags