Iran: Iwapo Trump ataachana na JCPOA atashangazwa mwenyewe
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i23836-iran_iwapo_trump_ataachana_na_jcpoa_atashangazwa_mwenyewe
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, iwapo rais mteule wa Marekani ataamua kuachana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, hatua hiyo itamduwaza na kumuweka kinywa wazi yeye mwenyewe.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Jan 18, 2017 13:27 UTC
  • Iran: Iwapo Trump ataachana na JCPOA atashangazwa mwenyewe

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, iwapo rais mteule wa Marekani ataamua kuachana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, hatua hiyo itamduwaza na kumuweka kinywa wazi yeye mwenyewe.

Mohammad Javad Zarif amesema hayo leo kwenye kikao cha Baraza la Uchumi Duniani huko Davos, Uswisi na kuongeza kuwa, kama Donald Trump aliyeshinda katika uchaguzi uliokuwa na utata mwingi wa mwaka jana huko Marekani ataamua kuachana na makubaliano ya JCPOA na kutaka kuanza mazungumzo mapya ya nyuklia ya Iran na kundi la 5+1, yeye mwenyewe atapigwa na bumbuwazi kwa hali atakayoiona.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amegusia namna mazungumzo ya nyuklia yalivyokuwa mazito, magumu na tata sana kati ya Iran na madola hayo makubwa duniani na kubainisha kuwa, Tehran imeamua kufuata siasa za uvumilivu na kuvuta muda na hadi hivi sasa haijaamua chochote kuhusiana na serikali ijayo ya Marekani. 

Donald Trump, rais mteule wa Marekani

 

Baada ya kumalizika mjadala huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amejibu maswali ya waandishi wa habari na kusema, hata kama Trump atataka kuachama na makubaliano ya nyuklia, kufanya hivyo hakutaifanya dunia kufikia mwisho.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran vile vile ameilaumu serikali ya Rais Barack Obama wa Marekani kwa kushindwa kutekeleza makubaliano ya JCPOA hususan kuhusiana na mabadilishano ya kibenki.

Amma kuhusiana na uchaguzi ujao wa Rais nchini Iran amesema, lililo muhimu ni kwamba wananchi wa Iran watapata fursa ya kutumia haki yao ya kidemokrasia kuchagua viongozi wanaowataka, na suala hilo ni muhimu mno duniani na katika eneo hili la magharibi mwa Asia.