Zarif: Shambulizi la Marekani dhidi ya Syria ni uzushi hatari sana
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa shambulizi la makombora lililofanywa na Marekani dhidi ya Syria ni kinyume na sheria za kimataifa na uzushi hatari sana.
Dakta Muhammad Javad Zarif ambaye alikuwa akizungumza na Waziri Mkuu wa Hungary, Zsolt Semjén aliyeko safarini mjini Tehran, ameashiria matukio ya siku za hivi karibuni nchini Syria na kusema: Iran inalaani mauaji ya raia wa Syria waliopoteza maisha kutokana na silaha za kemikali na vilevile mashambulizi ya makombora ya Marekani dhidi ya nchi hiyo ambayo yamekiuka sheria za kimafaifa na ni tukio hatari sana.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa, Syria ilipokonywa silaha zote za kemikali na Jumuiya ya Kuzuia Silaha za Kemikali (OPCW) lakini jumuiya hiyo haikukusanya silaha za kemikali za makundi ya kigaidi yaliyoko nchini humo. Ameongeza kuwa, kisingizio kilichotumiwa na Marekani kuishambulia Syria kitatumiwa vibaya na makundi ya kigaidi na kila mara yatakapojihisi kuwa dhaifu yatafanya mashambulizi kama hayo ya silaha za kemikali na kuzishirikisha pande nyingine kama Marekani katika vita vya Syria.
Akiashiria hatari ya kupanuka zaidi harakati na makundi ya kigaidi duniani, Dakta Zarif amesema kuwa: Kuna udharura wa kuimarishwa zaidi mwelekeo wa kuwepo mazungumzo na maelewano kati ya dini mbalimbali kwa shabaha ya kudhamini usalama na amani ya kimataifa.
Ikumbukwe kuwa alfajiri ya Ijumaa, Marekani ilivurumisha makombora 59 ya Tomahawk dhidi ya uwanja wa ndege wa Shayrat wa jeshi la serikali ya Syria huko Homs kwa madai yasiyothibitishwa ya kwamba Syria ndiyo iliyofanya mashambulizi ya silaha za kemikali kaskazini mwa nchi hiyo.